UDSM Kinara kwa utafiti Nchini

UDSM Kinara kwa utafiti Nchini

General / 25th October, 2022

Na Rajabu Msangi 

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimetajwa kuwa mstari wa mbele katika masuala ya utafiti ambao umekuwa na maslahi kwa Maendeleo ya taifa huku tafiti hizo zikiwa na michango chanya katika jamii. 


Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo  katika Kongamano la Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Miaka 40 ya Umahiri Katika Tathmini na Usimamizi wa Rasilimali na Mazingira, Kiser na Maendeleo ya Taifa. 


"Chuo hiki kimeendelea kuwa kinara kwa kutoa tafiti mbalimbali ambazo tunafahamu kwamba upande wa Sera zozote vizuri lazima ziwe zimefanyiwa tafiti za kutosha" Amesema Waziri Jafo. 


Aidha Dkt. Jafo amewataka wadau kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kukuza tafiti zinazohysu masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi. 


"Tafuteni wadau wengi ambao najua wapo tufanye tafiti nyingi za kimazingira za mabadiliko ya tabia ya nchi ambazo mwisho wa siku kwamba zitatusaidia katika mpango mzuri wa utengenezaju wa Sera katika sekta, wizara za kisekta mbalimbali kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu" Amesisitiza Mhe. Jafo 


Katika hatua nyingine Balozi wa Norway nchini Bi Elizabeth Jacobsen amesema Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kimekuwa na mahusiano mazuri na vyuo vingine nchini Norway na kujikita katika masuala ya utafiti huku akibainisha umuhimu wa kufanya Tafiti katika kuunda sera kwa maendeleo. 


"Tumejenga mahusiano makubwa ya utafiti na Maendeleo,  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaendelea kuwa mshirika mkubwa wa vyuo vya Norway,  utafiti ni muhimu sana ili kuandaa sera bora" Amesema Balozi Elizabeth 


Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam prof. William Anangisye amesema taasisi ya Tathmini Rasilimali imekuwa ikifanya utafiti katika masuala mbalimbali yanayohusu mazingira na hata kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kitaifa na hata kimataifa huku akisema tafiti hizo zimekuwa zikijenga uwezo nakukuza maarifa kwa ajili ya utungaji wa Sera katika ngazi zote nchini. 


Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Tathmini Rasilimali Prof. Joel Nobert amesema wafanyakazi wa taasisi hiyo wamekuwa mstari wa mbele katika kuratibu tafiti mbalimbali ikiwemo masuala ya maliasli, na hata katika masuala ya kijamii 


Awali Balozi wa Norway nchini Bi. Elizabeth Jacobsen amesema Norway itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam katika masuala ya Tafiti kwa maendeleo ya taifa huku akipongeza juhudi zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kufanya Tahiti nyingi zenye tija Kisera na maendeleo. 


Naye Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Anangisye amesema Tafiti hizi zinazofanywa na taasisi hii zinalenga kujenga uzoefu na kukuza uhusiano na Maendeleo ya kitaifa na kimataifa.