Uboreshaji wa haki za binadamu katika kuleta maendeleo nchini

General / 5th December, 2022

Serikali imesema uboreshaji wa haki za binadamu katika jamii ni hatua muhimu katika kuleta maendeleo nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkuu waWilaya ya Ilala Mhe. Ng’wilabuzu Ndatwa katika kongamano la kuelekea siku ya Haki za Binadamu lililofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na kukutanisha wadau mbalimbali wa haki za binadamu.

“Katika kuadhimisha siku hii ya maadili, haki za binadamu na mapambano dhidi ya Rushwa, majadiliano haya yatatusaidia kujua mahala tulipo kwa sasa, changamoto na nini cha kufanya ili kuhakikisha kuwa tunaendelea kulinda na kutetea haki za binadamu nchini.

Aidha Mhe. Ndatwa amesema uanzishwaji wa Taasisi zinazoshughulika na masuala ya Haki za binadamu ni muhimu kwa Serikali ili kuimarisha utulivu, amani na maendeleo kwa wananchi.

“Wajibu mkubwa wa taasisi hizi umekuwa ni kuhakikisha kuwa haki za binadamu, maadili na misingi ya utawala bora inazingatiwa na kuhakikisha kuwa rushwa inatokomezwa.

Naye Afisa Mfawidhi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora tawi la Dar es Salaam, Shoma Philip amesema lengo la kongamano hilo ni kujadili changamoto zinazokabili masuala ya Haki za binadamu, Utawala bora, Maadili Pamoja na Rushwa ili kupata suluhisho katika kutatua changamoto hizo na kuleta ufanisi katika utolewaji wa haki kwa wananchi katika misingi bora kwa maslahi ya Taifa.

“Tunatarajia kwamba wadau tuliowaalika maeneo mbalimbali wakiwemo Asasi za Kiraia, vilabu vya haki za binadamu watakuwepo kuziibua changamoto kama ambavyo wao wanaona katika maeneo yao, hivyo zitakavyojadiliwa tutaweza kujua nini tufanye ili tuweze kukabiliana nazo” Amesema Bi. Shoma


Kwa upande wake Mkuu wa dawati la Elimu kwa umma TAKUKURU Mkoa wa ilala, Elly Makala amesema kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika jamii ni chanzo cha uwepo wa ukiukwaji wa haki za binadamu na ukosefu wa maadili katika jamii.

“Mijadala hii kuhusu haki za binadamu ina afya kwa jamii kwa sababu wananchi wanapata nafasi ya kujifunza, kwa kuwa wakati mwingine Rushwa inatokea kutokana na Mwananchi kutojua haki zake za msingi, kwa hiyo ni kipindi ambacho tunatoa elimu kwa jamii na kuhakikisha kwamba wananchi wanajua haki zao msingi pale wanapoenda kupata huduma” Amesema Makala.

Katika hatua nyingine Kaimu Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi ya Umma, John Bakengesa amesema jukumu la kupinga Rushwa, Maadili Pamoja na kuimarisha Haki za Binadamu ni la jamii kwa ujumla na si kutegemea taasisi pekee.


Maadhimisho haya ya siku ya Haki za Binadamu  huadhimishwa kila mwaka huku mwaka huu wa 2022 yamebeba kaulimbiu inayosema “Maadili, haki za binadamu, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la Pamoja kati ya Serikal, wananchi na wadau wengine”.