Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kuleta manufaa kwa Utoaji wa Huduma bora

General / 1st December, 2022

Taasisi inayojihusisha na masuala ya Usafirishaji wa majini ya ISCOS imefanya mkutano wenye lengo la kuboresha huduma ya usafiri baina ya nchi zinazoundwa na taasisi hiyo ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Wakati akizungumza katika Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam,Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Gabriel Migire amesema  "Kikao hichi ni muhimu kwa sababu kinajaribu kubainisha changamoto  lakini kupendekeza njia mbalimbali au mbinu za kuweza kutatua changamoto ili kuboresha huduma katika ukanda wa Dar es Salaam".

Aidha amesema Mchakato wa kupata maoni na mapendekezo katika kikao hicho utasaidia  Utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam kuwa bora zaidi huku akiongeza kuwa hali hiyo itawafanya wadau kupata huduma bora katika usafirishaji.



"Ni Imani yetu kama serikali , kwa ushirikiano tunaoupata kutoka kwenye taasisi hii, na wadu kwa ujumla kunaweza kuifanya hii Bandari ya Dar es Salaam kufanya vizuri zaidi" Ameongeza Bw. Migire.

Hata hivyo Bw. Migire amesema Serikali inaamini kwamba juhudi zinazofanyika katika kuboresha Bandari hiyo zitazaa matunda mazuri kwa maslahi ya Taifa.

"Niipongeze sana ISCOS kwa juhudi hizi ambazo kwa pamoja zitasaidia kumhudumia huyu mteja , ambaye siku zote tunasema Mteja ni Mfalme" .

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ISCOS Daniel Kiange amesema lengo la kikao hicho ni kupokea taarifa ya utafiti uliofanywa na wadau wa Taasisi ya ISCOS kuhusu changamoto zinazoikumba Bandari ya Dar es Salaam hasa katika usafirishaji wa bidhaa ndani au nje ya nchi.

"Kwa hivyo kusudi hasa ni kwamba ,kufikia mwisho wa hiki kikao tutakuwa tumejadiliana kama washika dau, tujue shida ni nini, na tukuwe na mapendekezo ambayo Serikali zetu wanaweza kufanya ili zile changamoto ziwe zimeondoka, na Dar es Salaam iwe katika Ushindani "Competitive) katika Biashara katika ukanda huu wa Afrika'' Amesema Bw. Kiange.

"Kwa uchache tumegundua Kuna baadhi ya matatizo kwa upande wa usafiri ,pale mipakani kunakuwa na muda mwingi kwa mfano upande wa Kasumulu Songwe, tulitambua kwamba Teknolojia haitumiki sana, upande wa Tunduma, tuligundua Kuna Scanner moja ambayo haitoshi kwa sababu pale Kuna magari mengi yanapitia pale, kwahivyo inachukua muda sana kupita" Ameongeza .

ISCOS ni taasisi inayoshughulika na masuala ya Usafiri wa Baharini na inajumuisha nchi za Tanzania,  Kenya, Uganda, Zambia na DRC.