TIRA kuwafikia watanzania asilimia 50% ifikapo 2023

TIRA kuwafikia watanzania asilimia 50% ifikapo 2023

General / 4th July, 2022

Takwimu ya miaka mitatu iliyopita inaonyesha kuwa watanzania zaidi ya 15% wanatumia bidhaa mbalimbali za Bima hivyo mpaka kufikia mwaka 2023 Mamlaka ya usimamizi wa Bima (TIRA) wamepanga kuwafikia watanzania kwa 50%.

Hayo aliyasema jana Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware wakati akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika Banda la TIRA katika maonesho ya 46 ya Biashara ya sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine Dkt. Baghayo alisema Katika maonyesho ya sabasaba mwaka huu mamlaka ya usimamizi wa Bima nchini (TIRA) kwa kushirikiana na watoa huduma wao makampuni ya Bima, mawakala pamoja na washauri wa Bima wamekuja kutoa huduma mbalimbali za Bima ikiwemo kuandikisha wanachama katika huduma za aina mbambali za Afya, Magari, Nyumba, vifaa vya ndani na Biashara.

Pia Dkt. Baghayo alisema katika maonyesho hayo ya sabasaba wanatoa leseni kwa mawakala ambao wanaandikisha wanaotaka kujiunga kutoa huduma za Bima;

“Mamlaka imetoa miongozo ya kusajili wauza Bima ambazo tunazo hapa na watu wote wanaweza kuja kuzichukua, kuzisoma na kuangalia utaratibu wa kujisajili pamoja na miongozo ya huduma tunamiongozo ya takaful ya makampuni yanayotaka kusajili”

Mbali na hayo Dkt. Baghayo aliwashauri wananchi kukata Bima hasa bima binafsi ya Ajali ili kujilinda zaidi kiafya;

“Katika mamlaka tunashauri wananchi wanunue Bima zao binafsi, Bima za mtu mmoja wa tatu ni bima ambayo mfaidika anakua hajawahi kukata Bima bali ni mtu mwingine ndiyo amekata Bima, bima hiyo inaitaratibu fulani mrefu wa kuipata hivyo ni vizuri watanzania wanaposafiri kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine wakate Bima binafsi za ajali”

Aidha Dkt. Baghayo aliwakaribisha wananchi wote Tanzania kutembelea banda la TIRA, makampuni ya Bima, ofisi ya msuluhishi ili wapate taarifa mbalimbali ikiwemo ya kujiandikisha, kutoa malalamiko au madai, na kusajili kampuni mpya ili washiriki katika kuuza Bima