TIC na UNDP waandaa Kongamano la Kibiashara kwa sekta ya maendeleo
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. John Mnali amesema TIC kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Taifa linaloshughulikia maendeleo la UNDP pamoja na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara wameandaa kongamano la kuhamasisha na kukuza Uwekezaji na biashara kwa sekta zenye mrengo wa Maendeleo endelevu.
Ameyabainisha hayo leo Novemba 28, 2022 wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania jijini Dar es Salaam huku akisema kongamano hilo litafanyika tarehe 30 Novemba 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Rotana jijini Dar es Salaam.
" Lengo la mkutano huu ni kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zenye mrengi wa maendeleo endelevu kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani" Amesema Bw. Mnali.
"Fursa ambazo zipo katika sekta za kipaumbele zenye mlemgo wa maendeleo endelevu ni pamoja na sekta ya Kilimo na. Chakula, Miundombinu, Nishati, Elimu n.k" ameongeza.
Aidha amesema miongonu mwa manufaa ya kongamano hilo ni kusaidia na kuitangaza Tanzania kama miongoni mwa maeneo yenye fursa na mazingira mazuri ya kibiashara kwa kampuni mbalimbali duniani.
"Makampuni ya Tanzania yatapata fursa ya kuongea na Makampuni makubwa yatakayohudhuria na kupata nafasi ya kufanya biashara pamoja na kuweza kuingia ubia katika uwekezaji " Amesema Bw. Mnali.
Katika kongamano hilo Mgeni Rasmi anatarajia kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.