TASAC Yafafanua Juu Ya Tuhuma Zinazoendelea kwenye Mitandao
Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa
ufafanuzi kuhusu taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii hususani
Twitter na Instagram yenye malalamiko dhidi ya Shirika hilo kuhusu vijana zaidi
ya 400 waliokuwa TASAC wakipata elimu ya mafunzo kwa vitendo (intern)
Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Kaimu Mkeyenge, ametoa
taarifa hiyo leo March 10,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu taarifa hiyo na kutolea ufafanuzi kwa umma kuhusu vijana hao.
Mkeyenge amesema kuwa tuhuma walizotoa Vijana
hao ni pamoja na Kuvunjwa kwa mikataba bila kufuata
utaratibu, kufanya kazi bila bima ya afya na kwamba TASAC ilitoa rushwa kwa
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika mashauri ya kazi yaliyofunguliwa na
vijana hao ili haki isitendeke.
“Hakuna sheria inayomtaka muajiri yeyote yule
kumkatia bima ya afya kijana anayefanya shughuli za Mafunzo kazini suala hilo
halipo na hakuna taasisi yeyote inayoweza kufanya hivyo kwani stahiki zao
zimeainishwa kwenye Muongozo wa Kitaifa wa Mafunzo Kazi uliotolewa na Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemav”amesema Mkeyenge
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuwa kati ya vijana
209 waliofutiwa mikataba yao, ni vijana 41 tu ambao hawakuridhika na maamuzi
hayo ambapo vijana 32 kati ya vijana 41, shauri lao lilifutwa na CMA kwa kuwa
liliwasilishwa nje ya muda, hivyo ni vijana 9 tu ambao shauri lao dhidi ya
TASAC lilipokelewa na lipo katika Tume ya Usuluhisi na Uamuzi na vijana 168 waliobaki hawakupinga uamuzi wa
TASAC wa kuvunja mikataba yao kutokana na mabadiliko ya Sheria ambayo yalikuwa
ni nje ya uwezo wa Shirika.
Amehitimisha ufafanuzi huo kwa kusema kuwa TASAC ni
taasisi ya Serikali inayosimamiwa na Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali,
hivyo mashauri yake kisheria yanasimamiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
ikiwa ni pamoja na shauri hilo, hivyo Shirika halijatoa na haliwezi kutoa
rushwa yoyote kwa CMA ili kuzuia haki isitendeke kama ilivyoripotiwa katika
mitandao ya kijamii