Tanzania Kuunga mkono Mpango wa IMF utekelezaji wa mipango ya maendeleo
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Tanzania inaunga mkono mpango
ulioanzishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuingiza masuala ya
kijinsia kwenye utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.
Dkt. Nchemba ameyasema wakati akifungua mkutano wa
majadiliano kuhusu mkakati wa Shirika hilo wa kuingiza masuala ya kijinsia
kwenye mipango yake, uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wadau
mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa kwa upande wa Tanzania, Serikali
itaendelea kutilia mkazo masuala hayo ya kijinsia kwa kuwekeza rasilimali fedha
katika kuboresha afya ya mama na mtoto, utoaji elimu bila ada, na kuwawezesha
wanawake kiuchumi.
Aidha Dkt. Nchemba ameiomba jumuiya ya kimataifa
kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha masuala hayo na kusifu
ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na IMF ambapo ushirikiano huo umelenga
katika maeneo matatu ikiwemo kuelekeza bajeti kubwa kwenye maendeleo ya watu
kwa kuboresha makusanyo ya ndani kupitia kodi, kuboresha mazingira ya ufanyaji
biashara na kuimarisha usimamizi na matumizi ya fedha za Umma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Shirika la
Fedha la Kimataifa Mashariki (AFRITAC), Bi. Li Xiangming, amesema kuwa Uamuzi
wa Shirika lake wa kuingiza masuala ya kijinsia kwenye mipango yake umelenga
kujenga jamii yenye usawa na kuwawezesha wanawake kushiriki katika kujenga
uchumi na kupata maendeleo endelevu.
Aidha ametaja baadhi ya maeneo yatakayotiliwa
mkazo zaidi katika mkakati huo kuwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi,
kumiliki ardhi, kupata elimu bora na kupiga vita aina zote za ukatili wa
kijinsia zinazokwamisha maendeleo ya mwanamke na mtoto.