Tanzania Kufanya Biashara chini ya Mpango unaoongozwa na AfCFTA

General / 16th February, 2023

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Ally Gugu amesema, Tanzania iko tayari kufanya biashara chini ya Mpango wa Biashara Huria wa Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika.


Ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) uliolenga Uhamasishaji wa Sekta Binafsi kuhusu Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kuhusu Itifaki ya Biashara ya Bidhaa uliofanyika jijini Dar es Salaam.


"Warsha hii ni moja ya juhudi za muendelezo wa Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi tumekuwa tukifanya ili kuwaelimisha Watanzania hususan wafanyabiashara na wawekezaji nchini kuhusiana na fursa ambazo zipo ndani lakini pia kwenye eneo huru la biashara" Amesema Bw. Gugu 


"Sasa hivi Tanzania inaongoza kwa kuuza zaidi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na tupongeze Wafanyabiashara kwa kuichangamkia fursa hiyo ambayo Serikali kwa kushirikiana nao tumeipata, Lakini pia Tanzania inaongoza kwa kiasi kikubwa kwa kufanya biashara ikiwemo kuuza zaidi kwenye nchi za SADC,"Amesema Bw.Gugu 


Aidha amesema kuwa fursa hizo zinapaswa kuongezwa ili kusaidia Wafanyabiashara kuendelea kupata masoko na kuuza bidhaa zao katika soko kubwa la Afrika. 


"Nafasi yetu kama Tanzania kwa sasa kuuza Afrika bado iko chini, tuseme kwa ujumla wake na tunadhani kwa kupitia takwimu au chambuzi ambazo zimefanyika na wenzetu wa Benki ya Dunia, AfCTA itanyayua zaidi ya Waafrika wanaozidi zaidi ya Milioni 60 kuwatoa kwenye Umaskini " 


Kwa upande wake  Balozi Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC) Raphael Maganga amesema serikali inapaswa kuteleleza mikakati yake katika kuhakikisha Biashara ya Tanzania na Afrika inakuwa kwa ukubwa zaidi. 


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Nebart Mapwele amesema uwepo wa eneo huru la biashara kutaleta firsa kubwa kwa wafanyabisahara na kukuza uchumi nchini. 


"Kuna fursa kubwa sana katika kufanya biashara Afrika nasisi kama TCCIA tuko bega kwa bega kushirikiana na wenzetu kuhakikisha kwamba hizi biashara zinafanyika, na vibali tumeshaviandaa viko tayari,hivi vibali vitasaidia kwa mfanyabiashara kwenda kupata unafuu wa kodi" 


"Mpaka sasa hivi kuna nchi 8 ambazo zimekuwa kinara kama nchi za kuanzia Tanzania ikiwemo, lakini kuna wenzetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tunayo Kenya, Rwanda na wenzetu tunaona wameitikia kwa haraka, lakini Tanzania pia hatujachelewa tutumie hii fursa kusajili biashara zetu"