TANESCO yaeleza Mipango ya kupunguza Tatizo la umeme nchini
Na Rajabu Msangi
Ukame na matengenezo ya mitambo vimetajwa kuwa changamoto kubwa inayoikabili Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kusababisha upungufu wa umeme takribani Megawati 300 -350 kwa siku na kupelekea kuwepo kwa mgao kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Maharage Chande wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya hali ya umeme nchini katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere huku akisema kwamba kuanzia sasa watakuwa wanatoa taarifa Kwa umma kuhusu hali ya upatikanaji umeme na mipango inayoendelea katika kutatua changamoto hiyo.
“Changamoto hizi ndizo zimelifanya Shirika kushindwa kuwahudumia wateja wake kwa kiwango kilichokusudiwa. Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo lakini kuanzia Desemba hali ya upatikanaji umeme itakuwa imeimarika." Amesema Chande.
Katika kukabiliana na hali hiyo pamoja na mambo mengine yanayoendelea Bw. Chande amesema wanafanya maboresho ya mashine zake za ufuaji umeme kikiwemo kituo cha Ubungo 3 kinachotarajiwa kuingiza Megawati 20 katika gridi ya Taifa ndani ya siku mbili na zingine 20 mwanzoni mwa Desemba hivyo .
"Kituo cha Kidatu chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 50, matarajio ifikapo wiki ijayo Kituo cha Kinyerezi I, ifikapo mwisho wa mwezi huu kitatoa Megawati 90 ambazo zitaingizwa katika mfumo hivyo hivyo kwa pamoja kufanya jumla ya Megawati 220 kuingizwa katika gridi ya Taifa ifikapo kati kati ya Desemba." Amesema Chande.
Hata hivyo Chande wakati akielezea hali ya umeme nchini amesema usambazaji wa umeme kwa kituo cha Kihansi kinachozalisha megawati 180 kikiwa na maji kamili, kutokana na hali ya ukame, kwa sasa kinazalisha wastani wa Megawati 17 hadi 30, kikipoteza jumla ya Megawati 63 kutokana na upungufu huo wa maji.
"Kituo cha Pangani ambacho huzalisha megawati 68 kwa sasa kimezimwa kabisa, lakini pia Kituo cha Mtera kinachozalisha Megawati 80 kwa sasa kinazalisha Megawati 75. Lakini tunaamini kwa hatua tunazoendelea kuchukua umeme utapatikana kwa uhakika kuanzia Desemba .
Katika hatua nyingine amesema mikakati ya muda mrefu ni pamoja na kutumia bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 75, hivyo karibu linakamilika, kina cha Bwawa hilo ni kirefu hivyo maji yatakuwa ya kutosha na yatawesesha uzalishaji wa umeme wa uhakika.
Sambamba na hayo amesema juhudi za muda mrefu kwa kipindi cha miezi 18 ni kuhakikisha kuwa bwawa la umeme la Julius Nyerere linakamilika ambapo litaondoa kabisa adha ya umeme Tanzania.