Tahadhari dhidi ya wezi kupitia Mitandao ya mawasiliano

Tahadhari dhidi ya wezi kupitia Mitandao ya mawasiliano

General / 22nd March, 2023

Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini dhidi ya wezi wanaopita majumbani kwa madai ya kuwa ni watoa huduma kutoka katika mitandao ya mawasiliano huku wakijinasibu kutoa huduma mbalimbali kama vile kusajili laini za simu pamoja na kuwezesha laini kuwa na kasi zaidi ya intaneti katika matumizi ya simu janja kwani wezi hao hutumia njia zisizo rasmi ambapo baadae huishia kufanya uhalifu kwa kudukua taarifa za mteja na kufanya miamala mbalimbali ya simu.

Tahadhari hiyo imetolewa March 21, 2023 jijini Dar es Salaam na Msemaji wa jeshi la Polisi nhini SACP DAVID MISIME katika mafunzo ya siku moja ya Polisi jamii wa Mkoa, Wilaya na Kata kutoka Kanda Maalumu ya Dar es Salaam yenye lengo la kuwajengea uwezo kwenda kutekeleza majukumu ya Polisi kata katika maeneo waliyopangiwa.


 “Ukiona anakwambia kwamba toa laini yako kwenye simu nipe niweke kwenye simu yangu ili nikuunganishe na hiyo mifumo niliyokwambia kwa mfano kuongeza kasi ya intanenti, kusajili. Ukiona anakwambia toa line yako niweke kwenye simu yangu na anavyo endelea kumbe ameshapakua application ambayo inaweza ikanasa kumbu kumbu zako mpaka neno lako la siri huku akijifanya kugeukia pembeni, kumbe unapoweka neno au namba ya siri inaingia kwenye ile App anakuwa nayo. Ukiondoka anakwambia simu yako usiiwashe labda baada ya masaa 6 au masaa 12, utakapokuja kuiwasha utakuta meseji zinakwambia umehamisha fedha kupeleka sehemu Fulani, kumne umeshaibiwa”. Amesema SACP DAVID MISIME


Amesema, Jeshi la polisi linatoa tahadhari kwa wananchi kukataa kusikiliza watu wa namna hiyo lakini pia wananchi wameombwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi watakopokutana na jambo hilo. Sambamba na hilo SACP MISIME amesema baada ya kupatiwa mafunzo hayo jukumu kubwa ni kwenda kuzungumza na wananchi kwa ujenga urafiki na kushirikiana kukomesha matukio yote ya kihalifu.


Kwa upande wake mkufunzi katika Mafunzo hayo Dkt. Ezekiel Kyogo, amesema Mtanzania akielewa kwa undani somo kuhusu uzalendo itamsaidia kuchukia uhalifu na kutoa taarifa pale uhalifu unapotokea, na atakuwa balozi mzuri wa kutunza amani katika maeneo anayotokea.


Miongoni wa washiriki waliohudhuria mafunzo hayo ni pamoja na Mrakibu msaidizi wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi wa Temeke Glory Urassa ambae amesema mafunzo waliyopatiwa yatawasaidia kuibua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sehemu zao za kazi na kuzipatia ufumbuzi.

Jumla ya Askari wenye nyota moja hadi mbili waliopangwa kwenye kata ni 2372 na askari wa kawaida ni 1584 kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar Shehia zote 288 zimepangiwa wakaguzi wa kata na Askari Kata.