Serikali kupitia upya mkataba wa Songas

Serikali kupitia upya mkataba wa Songas

General / 18th May, 2022

Serikali imesema itapitia upya mkataba wa mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme ya Songas ili kuhakikisha kuwa haitakuwa na mkataba wenye dosari.

Mkataba wa sasa kati ya Serikali na Kampuni ya Songas utaisha muda wake Julai, 2024.

Hayo yamesemwa leo Mei 18,2022 na Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maluum Jesca Kishoa.

Kishoa amehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha inaingia mkataba mpya usiokuwa na dosari kwa manufaa ya wananchi kwa mwaka 2024.

Akijibu swali hilo Byabato amesema kuwa Serikali na Songas watakaa na kujadili mkataba mpya.

“Baadaye Serikali itajadili mkataba mpya na iwapo pande zote zitakubaliana, mkataba mpya wenye tija kwa Taifa na usio kuwa na dosari utasainiwa,”amesema

Amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) imeunda timu ya kupitia masuala ya msingi ya kuzingatiwa kwenye mkataba mpya kwa ajili ya maslahi kwa Taifa.

Katika swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya amehoji ni lini Serikali itapitia mikataba yote ili isipate hasara ikiwemo mkataba wa bwawa la uzalishaji umeme la Mwalimu Nyerere.

Akijibu swali hilo, Byabato amesema kwa niaba ya Serikali anachukua mawazo na maoni yaliyotolewa na wataendelea kushirikiana ya kufikia mikataba yenye tija kwa watu wote.

“ile ambayo imekwisha tutahakikisha tunafanya mikataba bora zaidi kwa nyakati zilizopo na ile inayoendelea tutaangalia namna ya kuifanya vizuri zaidi kwa manufaa ya wote,”amesema.