Serikali Kujenga Uwezo wa Viwanda vya Saruji – kuelekea Soko huru la Afrika (AfCFTA)

General / 22nd May, 2023


Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah (Aliye simama) akizungumza alipokuwa akitoa salamu za utangulizi na kuwakaribisha wadau wa Sekta ya Saruji katika mkutano huo.
Baadhi ya wadau walioshiriki kwenye mkutano huo wakimsikiliza Mhe. Waziri Dkt. Ashatu Kijaji.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema serikali itaendelea kuvijengea uwezo viwanda vya ndani vinavyozalisha Saruji kabla bidhaa hiyo haijaruhusiwa kuwa kati ya bidhaa kumi zitakazoweza kuingia katika soko huru la Afrika (AfCFTA).

Ameyasema hayo tarehe 21 Mei, 2023 mkoni Dar es salaam alipokutana na kufanya majadiliano  na wazalishaji na wasambaji wa saruji nchini katika kikao kilichojadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya viwanda nchini.

“Dhamira yetu ni njema kuendelea kujenga uwezo ili tutakapoingia na bidhaa hii tuwe na uwezo mkubwa wa kupeleka katika eneo kubwa la Afrika”.

 Aidha, Dkt. Kijaji amesema katika kikao hicho wamejadili kwa kina changamoto iliyopo ya upatikaji wa Clinker ambayo ni malighafi muhimu inayotumika kutengeneza saruji, ambapo amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto hiyo.

“Kumekuwa na Malalamiko ya upatikanaji wa clinker ndani ya nchi yetu ambapo wapo wachache ambao wanaochukua malighafii hii kutoka nje ya nchi hivyo kwenye kikao hiki tumejadiliana na kukubaliana ni kipi kinachosababisha wazalishaji wetu kuagia clinker nje ya nchi wakati viwanda vya ndani vina uwezo wa kuizalisha malighafi hiyo na kuuza nje ya nchi yetu.

Ameongeza kuwa uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini utawapunguzia gharama wazalishaji na kutengeneza ajira ndani ya nchi.

Amewahakikishia wazalishaji hao Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Bisashara kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati imeendelea kufanya kazi kuhakikisha viwanda vya ndani havikosi nishati hiyo muhimu.

Tanzania ina viwanda vya saruji 14 vyenye uwezo wa kuzalisha saruji tani milioni kumi, ambapo uwezo wa matumizi ya ndani ni tani milioni saba.

Kwa upende wake Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Kiwanda cha saruji Dangote Bw. Chux Mogbolu anaishukuru Serikali kwa kikao hicho muhimu ambacho kimejadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo upatikanaji wa malighafi ya Clinker.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha Saruji cha Nyati Bw. Sajiv Kumar amemshukuru Wizara kupitia waziri wake Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji kwa kuwasikiliza changamoto na maoni yao na kuhaidi kufanyia kazi kwa ajili ya maendeleo ya sekta hiyo.