Rais Samia: Hongereni NMB kwa mchango wenu katika Sekta ya Kilimo!
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Benki ya NMB kwa mchango uliotukuka kwenye Sekta ya Kilimo, Uvuvi, Ufugaji na Misitu, sambamba na kusapoti Program ya Kuandaa Vijana na Wanawake Kujenga Kesho Iliyo Bora (BBT). Rais Samia ametoa pongezi hizo leo alipotembelea Banda la NMB wakati akielekea kufunga Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa Benki ya NMB – Nsolo Mlozi, amemueleza Mheshimiwa Rais kuwa katika Sekta ya Kilimo (inayojumuisha kilimo chenyewe, Uvuvi, mifugo na misitu, NMB imeshatoa mikopo ya zaidi ya Shilingi Bilioni 319 tangu Julai 2021 walipoanza kutoa mikopo kwa riba nafuu ya asilimia 9 kwa mwaka.
Aidha alibainisha kuwa, NMB wameishatoa mikopo ya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.61 katika Sekta ya Kilimo katika kipindi cha miaka sita mfululizo, huku kwenye Programu ya BBT, tangu Machi wametenga Sh. Bil. 20. Pia, wanatoa Elimu katika Vituo atamizi kwa vijana na wanawake, ambao wamebeba kaulimbiu ya maonesho haya ya Nane Nane ambayo wameyadhamini kwa Sh. Milioni 80, huku wakishirikiana na Wizara ya Kilimo kuwezesha awamu inayofuata wanapoenda kwenye uzalishaji.
Mlozi alifafanua zaidi kuwa, katika Mikopo ya Kimkakati, NMB imetenga Sh. Bilioni 20 za mikopo ya ujenzi wa maghala nchi nzima ili kupunguza changamoto ya uharibifu na upotevu wa mazao ama kuathiri thamani na ubora wa mazao. Aliongeza kuwa wana mashirikiano na taasisi mbalimbali zinazotoa matrekta ‘power tillers,’ zana za kilimo na pembejeo, ikiwemo Kampuni ya Agricom Africa.
Kutokana na maelezo hayo Dkt. Samia aliipongeza NMB kwa namna inavyowajali na kuwathamini wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo, kisha akaiomba benki hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali yake katika kuboresha sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na misitu nchini .