Rais Samia Azindua Shule Ya Maandalizi Iliyojengwa Na Benki Ya NMB, Zanzibar

Rais Samia Azindua Shule Ya Maandalizi Iliyojengwa Na Benki Ya NMB, Zanzibar

General / 21st August, 2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akifungua Skuli ya Maandalizi Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa shamrashamra za Tamasha la Kizimkazi katika eneo la Makunduchi, Shehia ya Tasani Kusini Unguja, Zanzibar tarehe 20 Agosti, 2024.

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Agosti 20,2024 ameizindua Shule ya Maandalizi iliyojengwa na benki ya NMB katika eneo la Tasani, Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja Visiwani Zanzibar na kupewa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akiongea baada ya uzinduzi huo Rais Samia amesema “Sasa nitoe shukrani kubwa sana kwa NMB Bank kwa kufadhili ujenzi wa Shule hii lakini kama alivyosema Mtendaji Mkuu Bi. Ruth kwamba toka tumeanza hili Tamasha, NMB wamejitoa sana sio Shule hii tu kuna maeneo mengine wamejenga miradi inayofanana na hii, tunashukuru sanasana na tunategemea sana uwepo wenu na kazi yenu”

“Niwapongeze kwa kutambulika Duniani, nimesoma hilo jarida na nimesoma hiyo article wanatambulika kama benki bora inayojali mazingira, Jamii na utawala bora, hili la katikati la Jamii ndio hili mnaloliona sasa, na wanafanya hivyo kwasababu ni Jamii ndio inayowapa uwezo na wao lazima warudishe hisani kwa Jamii, kwahiyo hawakukaa na fedha wakahesabu faida tu na wao lazima wahakikishe kwenye faida wanatenga kiasi fulani wanarudisha katika Jamii”