Rais samia aiagiza wizara ya ujenzi na uchukuzi kuzingatia masharti ya mikataba katika ujenzi wa barabara

Rais samia aiagiza wizara ya ujenzi na uchukuzi kuzingatia masharti ya mikataba katika ujenzi wa barabara

General / 18th May, 2022


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuendelea kusimamia viwango vya ubora na kasi ya utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia masharti ya Mikataba.

Rais Samia ametoa wito huo wakati akizindua barabara ya Nyahua- Chaya yenye urefu wa kilomita 85.4 iliyojengwa kwa ushirikiano na Mfuko wa Maendeleo wa Serikali ya Kuwait (KFAED) kwa gharama ya shilingi bilioni 123.9.

Aidha, Rais Samia amesema barabara hiyo ina umuhimu kwa kuwa inaunganisha kanda mbalimbali za nchi ikiwemo ukanda wa magharibi, wa kati, kaskazini, kusini, eneo la maziwa makuu pamoja na nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kupitia Kigoma na Katavi.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa rai kwa wananchi kutokuhujumu miundombinu ya barabara pamoja na kuacha kutoa alama za barabarani kwa manufaa ya watumiaji kwa kuwa miundombinu hii inaigharimu Serikali fedha nyingi.

Rais Samia ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Tabora ikiwemo kwenye sekta ya elimu, umeme, mawasiliano ya simu, soko la tumbaku pamoja na miundombinu ya barabara.

Awali, Mhe. Rais Samia alisimama na kuzungumza na wananchi wa eneo la Kigwa, Wilaya ya Uyui akiwa njiani kuelekea kijiji cha Tura kwa ajili ya uzinduzi wa Barabara hiyo.

ZuhuraYunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.