NMB Yazindua Akaunti Ya NMB Pesa, Isiyokuwa Na Makato Ya Mwezi

NMB Yazindua Akaunti Ya NMB Pesa, Isiyokuwa Na Makato Ya Mwezi

General / 19th January, 2024

Na Mwandishi Wetu

Benki ya NMB imeanzisha kampeni kubwa ya kuhamasisha na kuwawezesha watu wengi kufungua akaunti ili waweze kunufaika na faida za kuwa sehemu ya mfumo rasmi wa fedha.

Kampeni hiyo inayoitwa “NMB Pesa Haachwi Mtu” ilitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki hiyo, Bw Filbert Mponzi, wakati wa kipindi cha Joto la Asubuhi cha Redio ya EFM.

Kiongozi huyo alisema lengo kuu la kampeni hiyo kupitia huduma ya NMB Pesa Akaunti ni kusaidia kuongeza idadi ya watu wenye akaunti za benki nchini na wale wanaohudumiwa na taasisi hiyo ambao sasa hivi ni zaidi ya milioni sita.

“Utafiti wa Finscope wa hivi karibuni unaonyesha kwamba kwa sasa ni watu asilimia 22 tu kati ya wale wenye sifa za kuwa na akaunti za benki nchini ndio wanazo, kiasi ambacho ni kidogo sana,” Bw Mponzi alibainisha kwenye kipindi hicho kilichorushwa moja kwa moja kutoka makao makuu ya benki hiyo.

Akifafanua, alisema NMB kama benki kinara nchini inawajibu wa kusaidia kutatua changamoto hiyo ndiyo maana ukafanyika uamuzi wa kuendesha kampeni hiyo inayowalenga hasa wananchi wa kawaida hususani mama ntilie, wamachinga na waendesha boda boda.

Katika kufanikisha zoezi hilo, Bw Mponzi alisema akaunti ya NMB Pesa inafunguliwa kwa TZS 1,000 tu na aina makato ya kila mwezi. Alisema lengo la unafuu huo ni kuondoa ile dhana ya kuwa kufungua akaunti ni jambo aghali linalohitaji fedha nyingi.

“Ufunguaji NMB Pesa Akaunti utafanyika kirahisi sana mahala popote kidijitali na maafisa mauzo wetu ambao ni maalumu kwa ajili ya kazi hiyo,” Bw Mponzi alibainisha.

“Kupitia mchakato huu, tunataka kutimiza ndoto za wale wote wanaohitaji kuwa na akaunti za benki,” aliongeza na kusisitiza kuwa NMB Pesa Akaunti ina faidi lukuki.

Faida hizo ni pamoja na kuunganishwa na huduma ya NMB Mkononi ambayo faida zake nyingi ni pamoja na mikopo ya Mshiko Fasta isiyokuwa na dhamana inayoaanzia TZS 1,000 hadi TZS 500,000.

Akizungumza baada ya kurushwa kwa kipindi hicho, Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi na Mauzo wa NMB, Bw Donatus Richard, aliwahasa wananchi kuitumia fursa ya NMB Pesa Akaunti kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.

Alisema hili kukidhi mahitaji ya soko, wataendelea kuja na bidhaa na huduma bunifu zitakazosaidia kutatua changamoto za kifedha za wananchi kama sehemu ya kuendeleza ajenda ya huduma jumuishi za kifedha nchini.