NMB yazindua akaunti ya kidijitali 'NMB Pesa Akaunti'
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Gabriel Makalla (kushoto) akipeperusha bendera pamoja na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara – NMB, Filbert Mponzi (kulia) wakiashiria kuzindua Rasmi NMB pesa Akaunti katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli Jijini Dar es salaam. NMB pesa Akaunti ni mfumo wa kidigitali wa ufunguaji wa akaunti wa benki ya NMB.
Benki ya NMB Imezindua suluhisho la kisasa ‘NMB Pesa Akaunti’ ambayo ni akaunti Ya kidijitali inayomwezesha mteja kufungua na kuanza kuitumia ndani ya dakika mbili tu, imezinduliwa leo stendi ya mabasi yaendayo mikoani ya Magufuli Bus Terminal.
Hatua hiyo kubwa inaongeza msukumo mpya katika jitihada za taifa za ujumuishwaji wa kifedha na upatikanaji wa huduma za fedha kidijitali kiurahisi.
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Bw Filbert Mponzi, sifa kubwa ya suluhisho la NMB Pesa Akaunti ni kuwa na mchakato mfupi wa kufungua akaunti mpya.
“Hii ni suluhisho yakusaidia kutatua changamoto za kifedha ambayo si tu ni akaunti inafunguliwa hapo hapo mteja alipo lakini pia utaweza kupata mikopo isiyo na dhamana, kutoa, kuweka au kutuma fedha, kulipia bili mbalimbali na kubwa zaidi haina gharama za ada za mwezi,” Bw Mponzi alisema.
Aliongezea kuwa pindi usajili wa mteja mpya unapokamilika, akaunti yake itafunguliwa mara moja na kuanza kutumika moja kwa moja wakati huo ikiruhusu upatikanaji wa huduma zote za msingi kama ile ya NMB Mkononi.
Bw Mponzi alimwambia Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw Amos Makala kuwa mwaka 2022 ulipoanza lengo la NMB lilikuwa ni kufungua akaunti mpya milioni moja. Mpaka sasa hivi zimefunguliwa 1,012,344. Hii ndio maana halisi ya huduma za kifedha jumuishi Tanzania
Jambo hilo limemfurahisha sana kiongozi huyo wa serikali ambaye kwenye hotuba yake alisema hii sasa ni fursa kwa Watanzania wote kuwa na akaunti ya benki. Ufunguaji huo wa akaunti unafanyika kwa msaada wa wafanyakazi wa mauzo wa benki hiyo kwa njia ya simu za mkononi za aina zote.
Umahiri wa ubunifu wa NMB na uwekezaji wake katika teknolojia mpya umeijengea heshima kubwa nchini benki hiyo na kuifanya itambulike kimataifa. Kwa mwaka huu pekee, NMB imeweza kujikusanyia zaidi ya tuzo 20 za kimataifa ilizotunukiwa na majarida yanayoheshimika duniani kama vile World Economic Magazine, Global Brands Magazine, International Banker Awards na International Business Magazine.
Ufunguaji huo mpya wa akaunti unafanyika mahala popote kwa Buku tu na hauhusishi kabisa karatasi ya aina yoyote na mfuguaji haitaji kwenda wala kufika katika matawi yao 228 yaliyotapakaa nchi nzima.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akimsikiliza Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki ya NMB, Filbert Mponzi wakati akimueleza juu ya mfumo wa malipo kwa kuskani QR (lipa Mkononi) ya Benki ya NMB katika moja ya Duka lililopo kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli mara baada ya kuzindua NMB pesa Akaunti ya Benki ya NMB.