NMB yapewa tuzo mwajiri bora Barani Afrika 2022.

General / 20th December, 2022

Kwa mara nyingine tena, Benki ya NMB imedhihirisha umahiri na ukubwa wake kiutendaji na kiundeshaji nchini baada yakufanikiwa kunyakuwa tuzo ya mwajiri bora barani Afrika – the Best Employer Brand Africa.

Ushindi huo mkubwa ulipatikana wiki jana mjini Port Louis huko Maurituis ambako NMB ilitunukiwa tuzo hiyo inayotambua umakini katika kuzingatia maslahi na maendeleo ya wafanyakazi na waandaaji wake ambao ni taasisi ya ajira ya Employer Branding Institute.

Akipokea nishani hiyo jana makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bw Filbert Mponzi, alisema tuzo hiyo ya nne ya mwajiri bora mwaka huu, ni ushahidi mwingine wa jinsi taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini inavyothamini wafanyakazi wake.

“Thamani ya wafanyakazi kwetu sisi NMB ni kubwa sana kwani wao ndiyo rasilimali inayoongoza na chanzo cha mafanikio yetu yote na tuzo mbalimbali ambazo tumekuwa tunazipata ,” Bw Mponzi alisema baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Afisa Mkuu Rasilimali Watu, Bw Emmanuel Akonaay.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB aliongeza kuwa baada ya kuongoza karibu kwa kila kitu nchini, sasa wameanza kupata mafanikio barani Afrika.

Hii inatokana na NMB kuzingatia matakwa ya msingi ya uongozi na uendeshaji taasisi hasa zile za fedha. Ushindi wa mwajiri bora, alifafanua, unatokana na NMB kutambua umuhimu wa rasilimali watu na kuwekeza katika maendeleo yake.

Mbali ya kuwa mwajiri bora, pia NMB ndiyo benki bora na kiongozi nchini. Mwaka huu tu, NMB imeweza kujikusanyia zaidi ya tuzo 20 za kimataifa ilizotunukiwa na majarida yanayoheshimika duniani kama vile World Economic Magazine, Global Brands Magazine, International Banker Awards na International Business Magazine. Mwezi jana, NMB alinyakua tuzo tatu za mwajiri mahiri kutoka kwa chama cha waajiri nchini (ATE) ikiwemo ile ya mwajiri bora wa mwaka 2022.

Bw Akonaay ambaye ndiye aliipokea tuzo ya Best Employer Brand – Africa huko Mauritius tarehe 13 mwezi huu alisema tuzo hiyo ni mwendelezo wa mambo makubwa ya NMB kwa mwaka huu. 

Akizungumza kabla ya kuikabidhi rasmi kwa Bw Mponzi, mtaalamu huyo wa ajira na wafanyakazi alisema heshima waliyopata inazidi kuifanya NMB kutambulika barani Afrika na duniani kote kwa ujumla.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa ushindi walioupata unatokana na juhudi za bodi na menejimenti ya NMB lakini zaidi wafanyakazi wa benki hiyo. NMB, alifafanua, imeonyesha kuwa si tu taasisi inayoongoza kwa huduma za kifedha bali pia ni kinara wa kujali maslahi ya wafanyakazi wake.

 “Sisi tunaongoza si tu kwa biashara na huduma bora bali pia linapokuja swala la rasilimali watu,” alieleza.