NMB, Yanga Wazindua kadi maalum za wanachama zenye Bima za Mamilioni
BENKI ya NMB na Klabu ya Yanga kwa kushirikiana na MasterCard Intenational, wamezindua Kadi Maalum ya Wanachama wat imu hiyo ‘NMB, Yanga World Debit MasterCard,’ ambayo mwanachama atailipia Sh. Mil. 1 kuipata, ikiambatana na faida kadhaa ikiwamo bima, seti ya jezi na tiketi 10 za VIP kwa msimu.
Hafla ya uzinduzi wa kadi hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam, ambako NMB iliwakilishwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, huku Rais wa Yanga Injinia Hersi Said na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo, Mzambia Andre Mtine wakiwawakilisha Wana Jangwani hao.
Akizungumza katika uzinduzi huo, ulioenda sambamba na kukabidhiwa kadi kwa wanachama waliolipia, Mponzi alisema kadi hiyo yenye nembo za NMB, Yanga na MasterCard, itakuwa na faida mbalimbali ikiwamo ukataji tiketi za ndege, bima za upotevu wa mizigo ama uahirishwaji wa safari za ndege.
“Ni kadi yenye faida lukuki, kwa sababu NMB hatujawahi kuja na jambo dogo, hatupoi. Ukishakuwa na kadi hii, utasafiri nayo kote duniani na unafanyia manunuzi na miamala mbalimbali kupitia ATM zote MasterCard duniani, ikiwamo ‘acces’ ya kukaa VIP Lounges katika Viwanja vya Ndege vya Kimataifa.
“Pia, NMB Yanga World Debit Black Card ambayo utaipata punde tu utafungua akaunti, ukiitumia kukata na kulipia tiketi ya ndege, utaingia moja kwa moja katika bima ya kupotelewa mizigo ambako utalipwa hadi dola 3,000 (takribani Shilingi Milioni 7.5), na endapo mizigo itachelewa, bima itakulipa hadi dola 300.
“Ukinunua tiketi kwa kutumia kadi hii, unapata hadi bima ya dola 7,500 ambazo ni karibu Sh. Mil. 20 ambazo utalipwa endapo safari za ndani na nje ya nchi zitaahirishwa na zaidi ya yote utakuwa sehemu ya huduma za NMB Mkononi na mikopo ukiwamo wa Mshiko Fasta usio na dhamana wala kujaza fomu,” alibainisha Mponzi.
Aliongeza ya kwamba, kadi hiyo itampa mwanachama wa Yanga punguzo la bei katika manunuzi ya migahawani, ‘supermarket’ na ‘petrol station kwa kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi, huku akitoa wito kwa Wana Yanga kujitokeza matawini kote nchini kufungua akaunti ama kulipia kadi hiyo.
Kwa upande wake, Injinia Hersi Said, licha ya kuishukuru NMB kufanikisha mchakato uliozaa kadi hiyo maalum, aliipongeza kwa mafanikio makubwa iliyopata benki hiyo mwaka jana 2023, ambako ilivuna faida kubwa inayoakisi thamani, ukubwa na ubora wa huduma zao, unaoendana na hadhi ya Yanga.
“Huu ni muendelezo wa masuala yanayoambatana na sherehe zetu za miaka 89 ya kuzaliwa kwa Yanga utakaofikia kilele Februari 11, tuko hapa kuzindua kadi ya kiwango cha juu kabisa katika huduma za kibenki Tanzania, kadi ambayo inamtambua mtumiaji wake kama Mteja wa Daraja la Juu.
“Ni heshima kubwa kwa Yanga kuona wanachama wetu wanapewa heshima ya kuwa ‘premium customers,’ hili ni zao la tathmini yetu iliyogundua kuwa wanachama wetu wanakosa huduma za ziada, ndipo tukaingia katika majadiliano na NMB yaliyozaa kadi hii,” alifafanua Injinia Hersi.
Aliongeza kuwa kuipata kadi hiyo mwanachama wa Yanga atatakiwa kulipia Sh. Mil. 1, na wao kama klabu wameiweikea thamani kubwa nyuma yake, ukiachana na zile zilizotajwa na NMB kupitia Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara.
“Ukiachana na faida zilizotajwa na NMB, sisi tutatoa kwa mwanachama atakayelipia kadi hii, ambako atapata tiketi 10 za Jukwaa la VIP kwa msimu mmoja, jezi seti sita (familia – mume/mke na Watoto wanne), pamoja na punguzo la kuanzia asilimia 10 ya gharama za matibabu katika Hospitali ya Aga Khan.
“Mwanachama mwenye kadi hii, atapata ‘special treatment’ kwa kila huduma za Yanga, ikiwemo jezi mpya za msimu toleo la kwanza linapoingia. Niwahakikishie Wana Yanga, kulipa Sh. Mil. 1 kunaipa thamani timu, lakini mrejesho wa huduma zetu kwao, ni mkubwa mno na wa thamani sana,” alibainisha.
Aliongeza kuwa, mapato yatokanayo na kadi hiyo na njia zingine, yanaenda kuihudumia klabu, hivyo kuwataka wanachama wa Yanga kushiriki ili kuiongezea thamani klabu yao na timu, huku akiishukuru NMB kuwapa thamani ya kuwa klabu ya hadhi ya juu, saw ana hadhi ya benki hiyo kinara nchini.