NMB yakabidhi vifaa madawati na vifaatiba Kilosa

NMB yakabidhi vifaa madawati na vifaatiba Kilosa

General / 29th August, 2024

Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka (katikati), Meneja wa Kanda ya Kati Benki ya NMB, Janeth Shango (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa, Michael Gwimile (wapili kulia) wakiwa na mashine ya kupimia shinikizo la damu (BP) baada ya benki ya NMB kutoa msaada wa madawati, viti, meza na vifaatiba kwa wilaya ya kilosa mkoani Morogoro.




Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka (katikati), Meneja wa Kanda ya Kati Benki ya NMB, Janeth Shango (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa, Michael Gwimile (wapili kulia) wakiwa na mashine ya kupimia shinikizo la damu (BP) baada ya benki ya NMB kutoa msaada wa madawati, viti, meza na vifaatiba kwa wilaya ya kilosa mkoani Morogoro.

BENKI ya NMB imekabidhi vifaatiba katika kituo cha afya Kimamba Pamoja na madawati, viti na meza vyenye thamani ya sh33.1milioni wilaya ya Kilosa ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wa benki hiyo kwa kurejesha faida inayoipata kwa jamii mkoani Morogoro.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kituo cha afya Kimamba na shule ya sekondari Chanzulu, Meneja wa Kanda ya Kati Benki ya NMB, Janeth Shango amesema moja ya vipaumbele vya benki hiyo katika kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto mbalimbali kwa kusaidia sekta ya elimu, afya na majanga pindi yanapojitokeza.

Shango ametaja vifaa vilivyokabidhiwa kwa uongozi wa wilaya ya Kilosa kuwa ni pamoja na madawati 235 kwa ajili ya shule nne za msingi za Dakawa Centre, Mbigiri, Malangali na Tindiga ambapo kila shule imepata madwati 65 huku shule ya sekondari Chanzulu ikipokea meza 50 na viti 50.

“Vifaa tulivyokabidhi ni moja ya ushiriki wetu kama benki katika kuunga mkono maendeleo ya jamii na tunao wajibu wa kuhakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika kutokana na faida tunayopata kurejea katika jamii kwa kutoa msaada sekta ya elimu, afya na majanga yanayojitokea kusaidia na kituo cha afya Kimamba NMB imekabidhi vifaatiba magodoro 60, mashuka 60 na mashine ya kupima BP.”amesema Shango.

Shango amesema kwa zaidi ya miaka 10 benki hiyo imekuwa ikitenga asilimia 1% ya faida na kuirejesha kwa jamii.

Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Kimamba, Dk Alfred Chiponda amesema wanaipokeza na kuishukuru benki hiyo kwa uongozi wake kuwapatia magodoro 60, mashuka 60 na mashine tatu za kupima shinikizo la dawa vikiwa na thamani ya sh8.1milioni.

“Tunaishukuru NMB kwa kupokea maombi yetu ya kuchangia upatikanaji wa vifaatiba na leo hii (jana) imetukabidhi magodoro ya wagonjwa 60, mashuka 60 na mashine tatu za kupima shinikizo la damu lakini bado tuna changamoto ya upungufu vifaatiba kikiwemo kti cha kisasa cha kutolea huduma ya kinywa na meno, mashine ya mionzi (X-Ray) tunahitaji taasisi nyingine ziweze kusaidia.”amesema Dk Chiponda.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema benki hiyo imekuwa msaada kwa wilaya hiyo kwa kuwajibika hasa katika kurejesha faida kwa jamii kutokana na faida wanazopata.

“NMB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwetu, imetushika mkono na kutupa faraja hasa baada ya wananchi wetu kukumbwa na mafuriko kipindi kile cha mvua za masika kwa kutupatia magodoro, tunawakushuru na leo hii (jana) tumepokea vifaatiba kituo cha afya Kimamba lakini shule zetu nne za msingi kukabidhiwa madawaji 235 na sekondari ya Chanzulu ikipokea viti 50 na meza 50.”amesema Shaka.

Shaka amesema ni wajibu wa kila mwananchi anayeenda kupata huduma ya kiafya kituo cha afya Kimamba kutunza vifaatiba hivyo huku walimu wakitakiwa kusimamia wnafunzi kutumia kwa uangalifu viti, meza na madawati ili kusaidia kupunguza changamoto wa vifaa hivyo shuleni.