NMB yaboresha Huduma za Makandarasi, sasa kukopeshwa hadi Bil. 5/- bila dhamana
BENKI ya NMB imezindua Maboresho ya Huduma za Kibenki kwa Makandarasi Wazawa, ambapo imefanya ongezeko la Kiwango cha Dhamana za Kuombea Kazi kutoka Sh. Bilioni 2.5 hadi Sh. Bilioni 5, huku ikiongeza pia Kiasi cha Dhamana za Miradi kutoka Sh. Bilioni 1.5 hadi Sh. Bilioni 3.
Maboresho hayo yanayokwenda kutengeneza mazingira mazuri ya ufanyaji kazi na ufanisi wa makandarasi wazawa, yametokana na utafiti uliofanywa na Benki ya NMB, ukilenga kuangalia uwezo wa makandarasi kifedha na jinsi gani wanavyokabiliana na ongezeko la mahitaji ya huduma za kikandarasi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema kasi ya ukuaji kiuchumi wa Taifa, unaenda sambamba na ongezeko la miradi ya ujenzi, huku makandarasi wazawa wakikosa zabuni za miradi mbalimbali kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.
“Ili kuhakikisha tunapanua wigo wa huduma katika kutatua changamoto za kifedha zinazowakabili makandarasi wetu, maboresho tuliyoyafanya yanajumuisha ongezeko la kiwango cha dhamana za Kuombea Kazi (bid bond) mpaka Sh. Bilioni 5 bila kuweka dhamana, kutoka Sh. Bilioni 2.5 za awali.
“Pia Tumeongeza kiasi cha Dhamana za Miradi (Performance Guarantee na Advance Payment Guarantee), kutoka Sh. Bilioni 1.5 mpaka Sh. Bilioni 3 kwa mradi mmoja, tena bila kuweka dhamana kwa Taasisi zote za Serikali kama vile Tanroads, Tarura, Ruwasa na nyingine,” alisema Mponzi.
Mbele ya mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, Mponzi alifafanua kwamba, maboresho hayo ni kwa makandarasi walio na miradi iliyo chini ya Serikali au taasisi za Serikali za pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Tanzania Bara na Zanzibar).
Na katika kuthibitisha mchango wa NMB kwenye Sekta ya Ujenzi, Mponzi alisema kuanzia mwaka 2022, wamekopesha zaidi ya Sh. Trilioni 1.1 katika mnyororo huo wa thamani, kiasi kilichokopeshwa kwa makandarasi zaidi ya 600 wanaotekeleza miradi mbalimbali nchini.
Mponzi alibainisha ya kwamba NMB imekuwa mshirika wa karibu na vyama mbalimbali, ikiwemo Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Chama cha Makandarasi Tanzania (TUCASA) pamoja na Chama cha Wanawake Makandarasi Tanzania (TWCA).
Akizindua maboresho hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, aliipongeza NMB kwa maboresho ya huduma zake kwa kundi hilo muhimu katika uendelezaji wa miundombinu nchini na kwamba ilichofanya ni kujibu kwa vitendo ombi la Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Niwashukurui sana NMB kwa sababu mnajibu kwa vitendo kile ambacho Rais Samia amekuwa akihimiza sana, cha kuwawezesha makandarasi wazawa kwenye sekta ya ujenzi inayojumuisha ujenzi wa barabara, reli, maji, umeme na kila kitu kinachotekelezwa na makandarasi wetu.
“Sisi kama Wizara tunatambua kuwa moja ya changamoto zinazowakabili makandarasi wazawa na kudumaza utekelezaji wa zabuni za miradi ni mitaji, kwa hiyo uwezo wao wa kupata miradi mikubwa umekuwa mgumu na athari za kuwatumia makandarasi wa nje ni nyingi pia.
“Kuendelea kuwatumia sana makandarasi wa nje, maana yake ni kwamba pesa yote badala ya kuibakisha mikononi mwa Watanzania ndani ya nchi, zitakuwa zinaondoka nje ya nchi kupitia makandarasi wa kigeni, hivyo kufanya mzunguko wa pesa ndani ya nchi kuwa mgumu.
“Kwa hiyo hiki kinachofanywa na NMB kwa Makandarasi, sio tu kinaenda kuwasaidia wao kupata miradi na kumaliza kwa wakati, bali pia ni kulisaidia taifa kubaki na pesa za ndani huku tukiwapa uwezo wazawa, ambao pia wanakabiliwa na changamoto ya vifaa ambayo inaenda kumalizwa na maboresho haya,” alisema.
Alisema hakuna namna inayowezesha kutekeleza miradi mikubwa pasipokuwa na menejimenti nzuri, hivyo akatoa wito kwa makandarasi nchini kuwa waaminifu katika kurejesha kile watakachokopa kutoka NMB, ambao wataenda kuwa msaada mkubwa kwao katika kukabiliana na ushindani na changamoto.