NMB, Wakandi waungana kuviwezesha Vyama vya Akiba na Mikopo
KWA kutambua umuhimu na mchango wa Vyama vya Akiba na Mikopo (Saccos) kwa maendeleo ya vikundi na mwanachama mmoja mmoja, Benki ya NMB imeingia makubaliano ya ushirikiano na kampuni inayotoa huduma za kifedha kigitali ya Wakandi Tanzania Limited, unaolenga kuleta suluhishi maalum za kibenki kwa vyama hivyo.
Makubaliano hayo yamezinduliwa jijini Dar es Salaam leo Jumatano Oktoba 9, ambapo kupitia ushirikiano huo, wanachama wa Saccos watachangia, kuweka akiba na kulipa mikopo yao kupitia njia NMB Mkononi, NMB Wakala na Matawi 231 ya benki NMB yaliyopo kote nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Teknolojia na Mabadiliko ya Kidigitali wa Benki ya NMB, Kwame Makundi, alisema kupitia masuluhisho maalum yaliyobuniwa, Saccos zitanufaika katika maeneo mengi, ikiwemo kupata taarifa za miamala ya akaunti zao kupitia mfumo maalum.
“Faida nyingine ni pamoja na Saccos kudhibiti mapato yao, kwani malipo yatafanywa kwa kutumia namba za malipo (control number), lakini pia zitaboresha ufanisi kwa kupunguza kazi na gharama za uendeshaji katika Saccos zilizo chini ya Wakandi Tanzania,” alisema.
Makundi aliongeza kwa kueleza kuwa, kwa mujibu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Ripoti ya Mwaka ya Utendaji wa Saccos na Usimamizi kwa Mwaka 2022, inaonesha kuwa kuna Vyama vya Akiba na Mikopo vilivyopata leseni kufikia mwaka huo vilikuwa 801.
“Idadi ya wanachama iliongezeka kutoka milioni 1.3 mwaka 2021 hadi wanachama milioni 1.8 mwaka 2022, sawa na ukuaji wa asilimia 38, hii inamaanisha kwamba hadi kufikia mwaka huu wa 2022, idadi hiyo imeongezeka sana na hii inaonesha jinsi Saccos zilivyo muhimu katika jamii yetu.
“Kwa mantiki hiyo suluhishi hizi ni muhimu kwa ustawi wa vikundi hivi, hasa ukizingatia kuwa Saccos zimekuwa na mchango mkubwa kwa watu binafsi, familia, wafanyabiashara, wajasiriamali, wafanyakazi kupanga mikakati ya maendeleo kupitia akiba na mikopo,” alisisitiza.
Makundi alibainisha kuwa, masuluhisho yatokanayo na ushirikiano baina ya MB na Wakandi Tanzania Limited, hayatoishia tu kubadili namna ya usimamizi wa fedha za vikundi, bali pia wanachama.