NHC yaingia Mkataba na KingJada Hotel Uwekezaji Morocco Square

General / 27th January, 2023

Na Rajabu Msangi 


Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)limeingia makubaliano kwa kutia saini na Kampuni ya Kingjada Hotel kwa ajili ya uwekezaji wa Hotel katika jengo la Morocco Square.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa upangishwaji na uwekezaji wa Ubia kati ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Kampuni ya KingJada Hotel iliyofanyika Morocco squares jijini Dar es Salaam.

"Hotel hii ipo mahali safi kabisa , kwa sababu ukiacha watu wa mbali kabisa itahudumia watu wa maofisi ya hapa, watu wanaokuja shopping mall, na watu wa makazi pia" Amesema Mchechu.

"Kwa sababu Morocco ipo katikati ya mji , ukiangalia mji wetu ulivyoenda kupanuka sasa hivi , maana yake hii ni Hotel ambayo, Mwekezaji yoyote itakuwa ni rahisi kwenda na kufanya shughuli zake na kumalizia mahitaji yake katika eneo hili" Ameongeza Bw. Mchechu.

Aidha amesema jengo hilo litakuwa na mjumuisho wa uwekezaji mchanganyiko " Hapa ilikuwa ni mchanganyiko wa vitu vinne , tunazungumzia ofisi, shopping mall, makazi pamoja na Hotel, na Kuna parking yakutosha ambayo magari zaidi ya 1000 yanaweza kupakiwa"

Hata hivyo Mchechu amesema ujenzi wa jengo hilo ulilenga watu wenye kipato cha kati na juu huku akibainisha majengo mengine ambayo yanajengwa na Shirika hilo yanalenga watu wa kati na chini.

"Kila tunapofanya ujenzi kuja kundi ambalo tunakuwa tumelilenga na mtu aside kuona kuwa kwa bei hii, hawa jamaa sio watu wetu sisi, hapana, sisi ni watu wa kila mtu kwa sababu National Housing tunapaswa kujenga majengo ya watu wa kipato cha juu, kati na chini, na wote ni wateja wetu". Amefafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni ya KingJada Hotels and Apartments Risasi Mwaulanga amesema endapo ubia huo utafuata sheria na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa mkataba huo ni sababu ya kufikia malengo makubwa.

"Tukifanya ubia na Shirika letu hili Pendwa kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa mikataba yetu, KingJada Hotels and Apartments tunayo imani Shirika litafika mbali kimalengo na kimkakati lakini na sisi Wabia wao kibiashara kufikia malengo yetu kibiashara" Amesema Mwaulanga.

Katika hatua nyingine ameongeza kuwa uwekezaji huu unachagizwa na jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu na juhudi za serikali kuweka mazingira mazuri ya Uwekezaji nchini.