NHC Yaingia Makubaliano na Benki ya Absa Tanzania

General / 18th February, 2023


Na Rajabu Msangi

Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi Mhe .DKt. Angeline Mabula amesema Uwekezaji katika sekta ya Nyumba unachangia katika ukuaji wa mitaji, ajira, afya na elimu huku akibainisha kuwa sekta hiyo ni kichocheo cha kukuza uchumi wa nchi.

Ameyabainisha hayo wakati akifungua mahusiano ya makubaliano kati ya Shirika la Nyumba la Taifa na Benki ya Absa Tanzania hafla iliyofanyika Morocco squares jijini Dar es Salaam.

"Serikali zote duniani zinathamini malengo ya sekta ya nyumba katika kukuza uchumi wa nchi na kichocheo cha kudumisha amani pia, kwa sababu kama huna nyumba au mahali pakulala maana yake hapatakuwa na amani " Amesema Dkt. Mabula.

Aidha Dkt. Mabula amesema Serikali kupitia sekta ya fedha imeendelea kufanya jitihada katika sekta ya nyumba ikiwemo suala la uanzishwaji wa Mikopo ya nyumba ambao ulipelekea kuanzishwa kwa Taasisi ya Mikopo ya Nyumba (TMRC) mwaka 2010 pamoja na mifuko midogo ya nyumba mwaka 2015.

"Hizi zote ni jitihada za serikali kutaka kumwezesha mwananchi wa kawaida kuwezesha kumiliki nyumba , Uanzishwaji wa Taasisi hizi kwa maana ya TMRC umewezesha benki na taasisi kadhaa kuweza kuwa na mitaji kwa ajili ya mikopo ya nyumba kwa ajili ya watanzania"


Katika hatua nyingine Dkt. Mabula amesema bado nchi inakabiliwa na uhaba wa nyumba hususani zenye gharama nafuu huku akipongeza Benki ya Absa kuja na bidhaa ambayo inawezesha watu kupata nyumba na kupunguza idadi ya uhitaji wa nyumba nchini.

"Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ambayo tumekamilisha mwaka jana Agosti, wote tunatambua kuwa Tanzania tuko Milioni 61,741,120 ambao kuna ongezeko la asilimia 3.2, na idadi ya majengo tuliyonayo ni Milioni 14, 348,572 ambapo majengo yasiyo ya ghorofa ni Milioni 13,540,363 sawa na asilimia  94.3 ya majengo yote nchini"

"Hivyo mahitaji ya nyumba bado ni makubwa, bado tunatakiwa pengine kuwa na nyumba zisizopungua 390, 981, na kwa rekodi za nyuma zilizokuwa Mchechu utakuwa ni shahidi,tulikuwa tunasema  tunahitaji walau nyumba laki mbili kila mwaka lakini kwa sensa iliyifanyika hivi karibuni, kwa hesabu ya haraka haraka  tunatakiwa kuwa na nyumba walau 390, 981 kwa mwaka" Ameongeza Dkt. Mabula.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Nehemia Mchechu amesema kuingia makubaliano na  Benki ya Absa ni sehemu ya kuyafikia malengo yao katika kuhakikisha watu wanamiliki nyumba nchini.

"Tuna ubia (partnership)na Mabenki 20 lakini niseme katika benki zote 20 tulizonazo , benki iliyowasoma na ikawaelewa watanzania vizuri ni Absa, kwahiyo nawapongezeni sana katika hilo" Amesema Mchechu.

Aidha ameongeza kuwa  Shirika lina miradi mingi na linaendelea kuwa na shauku kubwa katika maendeleo ya sekta ya Nyumba nchini .

"Miradi yetu mingi italenga sana soko la kati na chini kati, lakini soko la juu nao tutawapa vyao"

"Tuna Miradi ya Samia Housing  Scheme, ile ni miradi ambayo tunaenda kuijenga Tanzania nzima lakini msisitizo mkubwa upo Dar es Salaam na Dodoma na Mikoa mingine tutaenda kulingana na uhitaji, Nyumba za Kawe tumezianza hatujatoka hata juu ya msingi asilimia 70 zimeshauzwa" Ameongeza Bw. Mchechu.


Naye Mkurugenzi wa Benki ya ABSA Tanzania Abdi Mohamed amesema anafahamu changamoto wanazopata watu kuhusiana na ujenzi wa nyumba ambapo alitolea mfano wa uelewa mdogo kwenye suala hilo.


‘’ Watu wengi wanajenga nyumba kwa akiba wanayojiwekea na wengine huwachukua miaka kumi hadi kumi na tano kukamilisha ujenzi, Benki ya ABSA inachofanya ni kujenga uelewa kuwa watu wanaweza kuwa na nyumba kwa muda mfupi na kufanya malipo kidogo kidogo’’. Amesema Mohamed



Ikumbukwe Shirika la Nyumba la Taifa NHC lilizindua rasmi sera ya ubia Novemba 16, mwaka 2022 na kuzinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakishirikiana na sekta binafsi ambapo sera hiyo ilifanyiwa maboresho mbali mbali na kueleza kutoingia ubia na sekta binafsi zaidi ya miaka (10)likuwa ni pamoja na kuangalia Sera ambayo inaweza kuvutia wawekezaji na kukuza pato la Taifa.