NBC na Jubilee Allianz Kutoa Mafunzo kwa Mawakala

NBC na Jubilee Allianz Kutoa Mafunzo kwa Mawakala

General / 10th February, 2023

Benki ya NBC kwa kushirikiana na kampuni ya BIMA Jubilee Allianz imesema hadi kufikia mwezi wa sita wanatarajia kutoa mafunzo kwa mawakala wasiopungua 6000, lengo likiwa ni  ni kuongeza urahisi wa upatikanaji wa Bima nchi nzima, kukuza soko la Bima pamoja na kutoa elimu ya bima .

 

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa kitengo cha Bima Kutoka NBC, Benjamin Nkaka wakati wakikabidhi vyeti kwa mawakala wa Benki ya Biashara NBC zaidi ya 100 waliofanya mtihani na kufaulu ikiwa ni wiki chache zilizopita baada ya kukamilika kwa zoezi la kupatiwa mafunzo ya uuzaji Bima.

 

“Kampuni ya Bima ya Jubilee Allianz kushirikiana na Benki ya NBC, ilichagua mawakala wa huduma za kifedha, kuwadhamini na Kuwapeleka mafunzo ya muda mfupi katika chuo cha Africa College of Insurance and Social Protection kwaajili ya kupatiwa elimu ya Bima.” Amesema Nkaka

 

Aidha, Nkaka amesema kuwa anatarajia kuona wahitimu hao wanatoa huduma bora kwa wateja, kuwapatia elimu na uhakikisha kuwa wanasogeza zaidi huduma ya BIMA kwa wateja wao.

 

Kwa upande wake Meneja Mkuu msaidizi wa Jubilee Allianz, Abullatif Suleiman, amesema ukuaji wa soko la bima kwasasa ni mdogo na hivyo Jubilee Allianz pamoja na Benki ya Biashara NBC wameamua kutoa mafunzo ili kukuza huduma ya kuuza Bima.

 

“Sisi kama Jubilee Allianz tunaona ni fursa kubwa, nyinyi mnapokea wageni wengi katika vituo vyenu na katika hili hatutowaacha pekeenu, sisi na NBC tutakuwa tunawapitia katika vituo vyenu kuhakikisha mnaweza kuuza na kutatua changamoto mnazokutana nazo” amesema Abullatif

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mafunzo na taaluma kutoka ACISP, Ansium Anseum amesema, chuo hicho kitahakikisha kinaendelea kutoa mafunzo na kuwawezesha mawakala kutoa huduma bora za bima nchini.

 

Katika hatua nyingine amewataka wahitimu hao kutoa huduma iliyo bora kwa kuzingatia maadili ya kazi na misingi iliyowekwa kwani huduma ya bima inahitaji uwazi na ukweli kwa mteja.

 

Mpaka hivi sasa Benki ya NBC ina zaidi ya mawakala 9500 ambao wapo nchi nzima wakiwemo mawakala wakuu, wa kawaida na mawakala wa kati.