NAIBU KATIBU MKUU WA MAZINGIRA APONGEZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI KISHAPU

NAIBU KATIBU MKUU WA MAZINGIRA APONGEZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI KISHAPU

General / 13th August, 2023

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dr. Switbert Mkama amesema ameridhishwa na usimamizi na utekelezaji wa Mradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo Mfumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Amesema hayo alipofanya ziara ya kukagua mradi wa mashine za kukoboa na kusaga nafaka, madume bira ya ng‘ombe aina ya borani na hatua za uchimbaji wa malambo zilizopo katika vijiji vya Kiloleli na Muguda wilayani humo tarehe 12 Agosti 2023.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, Dkt. Mkama ametoa wito kwa wananchi wilayani humo kuitunza miradi hiyo ambayo inakelezwa kwa lengo la kusaidia katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na ukame kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Ndugu zangu naomba niwaambie miradi hii inayoletwa hapa kwenu na maeneo mbalimbali itawasaidia katika kujipatia kipato kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo ufugaji nyuki zitawasaidia kuacha shughuli zinazoharibu mazingira zikiwemo ukataji miti na kuchoma mkaa na mkipata fedha mtanunua majiko banifu na ya gesi,“ alisema.

Aidha, Dkt. Mkama aliwahimiza viongozi na wananchi wilayani humo kuhakikisha shughuli zote za mradi zinakamilika Desemba 2023 wakati utakapofikia ukingoni pamoja na kuufanya kuwa endelevu iweze kuwanufaisha kwa vizazi vijavyo kwa vile unatarajia kufikia ukingoni Disemba 2023.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutekeleza Mradi wa EBARR akisema kwamba umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wilayani humo.

Alisema miradi mbalimbali ikiwemo malambo, mifugo, kiwanda kidogo cha uchakataji wa ngozi ambacho kinahusisha kikundi cha ushonaji wa viatu na unenepeshaji wa mifugo unakwenda kuinua ufugaji wilayani humo. 

Pia, mbunge huyo alisema kuwa mashine za kukamua alizeti zinazotarajiwa kutolewa kupitia mradi huo zitaweza kuwasaidia wakulima wa zao hili kupata fursa ya kukamua mafuta na hivyo kuinua uchumi wa wilaya.

Shughuli hizo zinazotekelezwa kupitia Mradi wa EBARR wilayani Kishapu zinagharimu shilingi bilioni 1.6 ambapo unatekelezwa katika Kata ya Kiloleli inayohusisha vijiji vya Kilollei na Muguda na Kata ya Lagana katika vijiji vya Mihama na Beledi.

Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Nchi zinazoendelea kupitia Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) unatekeleza pia katika wilaya za Simanjiro (Manyara), Mvomero (Morogoro) na Kaskazini ‘A’ Unguja (Zanzibar),

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama(mwenye miwani) akipata maelezo kuhusu mradi wa madume ya ng’ombeaina ya golani na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya WilayaKishapu Bw. Sabinus Chaula alipotembelea Mradi wa Kuhimili Mabadiliko yaTabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Halmashauri yaWilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga tarehe 12 Agosti, 2023.


Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama(mwenye miwani) akikagua maendeleo ya ujenzi wa birika la kunywesheamifugo katika Kijiji cha Kiloleli alipofanya ziara ya kukagua Mradi wa KuhimiliMabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR)unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.