Nafasi za Kazi JWTZ, Watakao Tumia Ujanja Kuzipata Waonywa

General / 9th March, 2023


Jeshi la wananchi la Tanzania limetangaza nafasi za kujiunga na jeshi kwa vijana wa kitanzania wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi shahada ya uzamili ambao wamemaliza mkataba wa miaka miwili wa mafunzo ya kujitolea katika jeshi la kujenga taifa (JKT) na kurudishwa majumbani.


Hayo yamebainishwa leo Machi 9,2023 Jijini Dodoma  na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na uhusiao wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda , wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema nafasi hizo zinawahusu vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha 4 na cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.


"Nafasi hizi haziwahusu vijana ambao bado wapo katika kambi mbalimbali za JKT kwa sasa bali zinawahusu wale ambao tayari wamemaliza mikataba yao ya mafunzo ya miaka miwili na kurudishwa majumbani na wenye vigezo vilivyotajwa vya kuomba nafasi hii," amesisitiza Luteni Kanali Ilonda


Aidha,Luteni Kanali Ilonda, ameeleza vigezo vitakavyozingatiwa wakati wa katika maombi hayo kuwa mwombaji awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa mwenye kitambulisho cha Taifa,awe na afya nzuri na akili timamu,awe na cheti halisi cha kuzaliwa,vyeti vya shule nav yeti vya taaluma.


Vigezo vingine ni pamojana na awe hajatumikia Jeshi la Polisi,magereza,Chuo cha Mafunzo au Kikosi maalumu cha kuzuia magendo na asiwe ameoa au kuolewa.


Kwa upande wa utaratibu wa jinsi ya kutuma maombi Luteni Kanali Ilonda ,amebainisha kuwa maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe makao makuu ya jeshi hilo Dodoma kwanzia leo tarehe 9,Machi hadi tarehe 20 ,Machi 2023 yakiwa na viambatanisho kama vile nakala ya kitambulisho cha taifa au namba ya nida,nakala ya cheti cha kuzaliwa,vyeti vya shule na chuo,nakala cheti cha JKT na namba ya simu ya mkononi ya muombaji na maombi yanaweza kutumwa Kupitia njia ya barua pepe ulinzimagazine@tpdf.mil.tz


Pia Luteni Kanali Ilonda amewataka wananchi kuwa makini na matapeli kwani kumekuwa na tabia ya kuibuka matapeli pindi matangazo hayo ya nafasi ya kujiunga na jeshi hili zinapotangazwa


"Natambua katika matangazo haya ya kujiunga na nafasi hizi kuna matapeli watajitokeza na kuanza kupenyeza utapeli wao ,hivyo watanzania wasidanganyike wala kurubuniwa na hakuna njia ya mkato katika kupata nafasi hizi zaidi ya kuzingatia vigezo vilivyowekwa wazi kabisa' amesema Luteni Kanali Ilonda