MV Mwanza kufungua Masoko ndani na nje ya nchi

MV Mwanza kufungua Masoko ndani na nje ya nchi

General / 14th February, 2023

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema serikali iliamua kujenga meli kubwa katika Ziwa Victoria ili kukidhi mahitaji ya soko yanayotarajiwa kuongezeka baada ya kukamilika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete jijini Mwanza wakati wa hafla ya kuitoa meli ya Mv Mwanza ‘Hapa kazi tu’ na kuiingiza majini kuashiria kukamilika kwa ujenzi wa umbo la chombo hicho cha kisasa ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 82.

“Kujengwa kwa meli hii kutasaidia kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha safari mpya zitakazosaidia kurahisisha shughuli za kibiashara, kikazi, utalii na safari binafsi kwenye maeneo mengi zaidi kuliko ilivyo sasa” amesema Mwakibete.

Aidha ameongeza kuwa ujenzi wa meli hiyo ukikamilika utaboresha usafiri kwenye maziwa makuu kwa kutoa huduma katika bandari za Kisumu nchini Kenya, Kemondo na Bukoba mkoani Kagera, Jinja na Port Bell nchini Uganda, Musoma mkoani Mara na Mwanza.

Katika hatua nyingine ameaigiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) iziboreshe bandari katika Ziwa Victoria ili meli hiyo itie nanga bila tatizo na ifanye kazi kwa ufanisi.

Awali Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSC), Eric Hamissi amesema meli hiyo yenye urefu wa mita 92.6 na upana wa mita 17 ni kubwa zaidi katika maziwa makuu yote Afrika.

Hamissi ameongeza kuwa meli hiyo yenye ghorofa tano itakuwa na lifti yenye uwezo wa kubeba watu 20 kwa wakati mmoja ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari zaidi ya 20 kwa wakati mmoja huku akibainisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 109.15 na inajengwa na Watanzania zaidi ya 300 wenye umri wa miaka 21-35.