Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi Kuanza Mwakani

General / 24th November, 2022

Na Rajabu Msangi.

Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi unatarajiwa kuanza mwaka kufuatia hatua ya serikali ya Tanzania kusaini mkopo na Benki ya Dunia ikiwa ni katika kutatua changamoto inayowakabili wakazi wa Dar es Salaam katika bonde la mto huo.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Miradi ya Benki ya Dunia chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Humphrey Kanyenye wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Millenium Tower jijini Dar es Salaam kuhusu Mradi huo wa Bonde la Mto Msimbazi.

"Mkopo huu unakwenda kufanya kazi ya ujenzi wa daraja lakini pia zinakwenda kujenga kingo za mto kuanzia katika hili eneo la chini la mto Msimbazi lakini pia Kuna kazi nyingi zinaenda kufanyika ikiwemo kupanda miti kuanzia Pugu ili kurudisha ule uoto wa asili uliokuwepo toka mwanzoni" Amesema Mhandisi Kanyenye.

Aidha amesema serikali inaelekea kujenga maeneo yatakayokuwa yanahifadhi mchanga katika harakati za kupunguza mchanga mwingi ambao unakwenda katika daraja la Jangwani.

"Mpaka sasa hivi tuna tani zaidi ya Milioni nne na laki tatu ambazo zimeshajirundika pale ambazo pia itabidi kuondolewa, ule mchanga utakaondolewa pale ndiyo utakaotumika kujaza kwenye lile eneo la Jangwani lote ili liweze kutumika kama lilivyokuwa linatumika hapo zamani"

Katika hatua nyingine Mhandisi Kanyenye amesema Kaya 3,800 ambazo zina watu 11,000 zinatarajia kulipwa fidia kwa ajili kupisha ujenzi wa mradi huo.

"Wananchi wanaambiwa mapema kabisa, kiwango cha pesa ambazo watalipwa na hakuna ambaye atalipwa pesa 'cash' taslimu, wote itabidi wafunguliwe akaunti pesa ziingie kwenye akaunti zao" Amesema Mhandisi Kanyenye.