Mpango awaomba NMB kueneza Elimu ya Bima kwa watumia Vyombo vya moto

Mpango awaomba NMB kueneza Elimu ya Bima kwa watumia Vyombo vya moto

General / 27th August, 2024

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango ameisihi benki ya NMB kuwafikia watu wengi zaidi kwa ajili ya kuwapa elimu ya Bima hasa waendeshaji na watumiaji wa vyombo vya moto.

Dk Mpango ametoa kauli hiyo Agost 26,2024 alipotembelea banda la maonyesho la NMB katika maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambayo kilele chake kimefanyika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Benki ya NMB kwa kushirikiana na kampuni za Bima za Sanlam na Reliance walikuwa wadhamini wakuu kwenye maadhimisho hayo huku ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo kwa benki hiyo kuwa mdhamini mkuu wa maadhimisho hayo.

Makamu wa Rais amesema suala la Bima kwa watumiaji wa vyombo vya moto ni muhimu lakini watu wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu huo jambo alilosema NMB inao uwezo wa kuwafikia Watanzania wengi na kwamba inaaminika.

“Watu wengi hawaoni thamani ya Bima, mtu akikata bima mwaka wa kwanza hadi miaka minne anaona hakuna tatizo basi anaacha, ninyi NMB mnaweza kuifanya kazi hiyo vizuri, niwatake mkaifanye kwani kinga ya chombo cha moto ni Bima na si vinginevyo,” amesema Dk Mpango.

Amesema baadhi ya watu wanaona kuwa Bima inawanufaisha mabenki na makampuni wakati si kweli, hivyo akaomba elimu zaidi ipelekwe hasa kwa waendesha pikipiki maarufu Bodaboda ili wajiunge na kusema NMB ni mahali sahihi kufanya hivyo.

Mkuu wa Idara ya Bima kwa benki ya NMB, Martin Massawe amesema ndani ya benki hiyo kuna mfumo wa kuwawezesha watumiaji wa vyombo vya moto kukata Bima kwa gharama ndogo inayobebeka.

Massawe amesema benki hiyo inatoa bima hadi ya Sh200 kwa mwezi huku watumiaji wa vyombo vya moto wakitakiwa kukata bima ya kuanzia Sh10,000 kiasi ambacho kinawezekana kwa kundi hilo kwa kumudu kulipia.

Kwa mujibu wa Massawe, NMB imefanya mazungumzo na viongozi wa madereva nchini ambapo mwikitio ni mzuri kwani wengi wameshajiunga na kukata Bima za vyombo vyao na bima za Maisha yao lakini akakiri kupokea maagizo ya kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu zaidi.

Akitoa salama kwa niaba ya wadhamini wengine, Massawe amesema wiki ya nenda kwa usalama barabarani wameipa kipaumbele na ndiyo maana wamebeba jukumu la udhamini kwa mwaka wa tatu.

Massawe amewaomba Watanzania na wakazi wa Dodoma kutembelea matawi ya NMB maeneo yote ili wapate fursa nyingi ikiwemo mikopo kwa ajili ya vyombo vya moto na biashara kwa masharti rafiki ambayo benki inazingatia kwa Maisha ya Wananchi.

 

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango (katikati) akimkabidhi Mkuu wa Idara ya Bima wa Benki ya NMB, Martine Masawe (Kulia) Tuzo ya kutambua mchango wa Benki ya NMB katika kufanikisha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani na miaka hamsini ya baraza la taifa la usalama barabarani kama mdhamini mkuu. Kushoto ni Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni.