Mikakati Mipya Kuzuia Ugonjwa wa Figo Nchini

Mikakati Mipya Kuzuia Ugonjwa wa Figo Nchini

General / 10th March, 2023

Serikali imejipanga kuweka jitihada za pekee ili kudhibiti na kuzuia ugonjwa wa figo na magonjwa yasiyoambukiza kwa ujumla kwa kuimarisha afua za kinga kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.


“Hapa naomba nikumbushe umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kupunguza matumizi ya vilevi na kuzingatia ulaji wa mlo kamili wenye mbogamboga na matunda ya kutosha ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa”amesema Makuwani.Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Mama na Mtoto, Dtk. Ahmad Makuwani, wakati wa Maandimisho ya Siku ya Figo duniani yenye kauli mbiu, . “Afya ya Figo kwa Wote,Kujitayarisha kwa yale yasiyotarajiwa ,kusaidia waliohatarini “yenye lengo la kuongeza ufahamu na elimu wa afya ya figo na kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima afya ambapo hadi kufikia Januari 31, 2023 wagonjwa 3,250 wanapata huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na wagonjwa 335 wamepandikizwa figo.


Dkt. Makuwani amebainisha kuwa hadi hivi sasa kwa mujibu wa tafiti ilizofanyika zimebaini kuwa amesema tafiti zimebaini kuwa takribani Watanzania 5,800 mpaka 8,500 wanahitaji huduma za kusafisha damu (dialysis)au huduma za kupandikizwa figo, na kwamba hadi kufikia Januari 31, 2023 wagonjwa 3,250 wanapata huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na wagonjwa 335 wamepandikizwa figo.


“Kati ya wagonjwa waliopandikizwa figo, wagonjwa 103 wamepandikizwa nchini, ambapo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepandikiza wagonjwa 70 na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma imepandikiza wagonjwa 33”amesema Dkt Makuwani.


Aidha, amehimiza kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha angalau kiasi cha lita 2.5 ya maji kwa kila siku na kujiepusha na matumizi ya dawa ambazo hazijatolewa maelekezo ya kitaalam na daktari.


Makuwani amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani(WHO)zinabainisha kuwa asilimia 10 ya watu wote duniani wanaishi na ugonjwa sugu wa figo ambapo tatizo ni kubwa zaidi kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 75 au zaidi huku karibu nusu yao wana tatizo hili.Kuhusu utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, Dkt Makuwani amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, serikali imeanzisha huduma za uchujaji wa damu kwenye hospitali za mikoa 8 kwa kuzipatia mashine 49 za dialysis na kukarabati majengo kwa gharama ya Tsh.Bilioni 2.8.


Siku ya Figo Duniani huadhimishwa kila Alhamis ya Wiki ya Pili ya mwezi Machi kila mwaka ambapo Jumuiya ya Kimataifa ya Nefrolojia (ISN) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Figo Duniani (IFKF)ilianzisha maadhimisho haya ambayo yalifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2006, kwa mwaka huu 2023 kitaifa imeadhimishwa Jijini Dodoma