MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI UTASAIDIA KUIMARISHA UTENDAJI-DKT YONAZI
Na; Mwandishi Wetu - Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt Jim Yonazi amesema, mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali ni mfumo mahususi wa uboreshaji wa utendaji Serikalini kwa lengo la kuona ni namna gani Rasilimali za Serikali zinaboreshwa na Kutumika vizuri.
Hayo ameyasema Mapema leo Terehe 4 Septemba Ofisini kwake Jijini Dodoma alipokuwa katika mahojiano maalum na chombo kimoja cha Habari, katika kuelekea Kongamano la wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika Jijini Arusha Wiki Ijayo, ambapo Dkt. Yonazi ameeleza kuwa, Uratibu wa Shughuli za Utendaji wa Serikali katika eneo la Ufuatiliaji na Tathmini una nia ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali unafanikiwa na malengo yanafikiwa.
Aliendelea kusema kuwa Dhana hii, ni dhana ambayo inalenga katika kuangalia utekelezaji wa Miradi ya Serikali Nchi nzima na kuona kama malengo yaliyowekwa katika Miradi hiyo yanafanikiwa. “Ili malengo hayo yaweze kufanikiwa ni lazima tufanye Ufuatiliaji tujue nini kinaendelea, tufanye Tathmini dhidi ya ile mipango ambayo ilikuwa imewekwa, lakini vilevile tuangalie kwamba tunajifunza nini kutokana na kile ambacho tumekiona kutoka katika Ufuatiliaji na Tathmini,” Alifafanua.
Aidha, Dkt. Yonazi Alimshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na wazo la kuanzisha mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini Nchi nzima,na kuweka vitengo na Idara mahususi kwa ajili ya kazi hiyo katika Wizara na Taasisi za Serikali kwa lengo la kuzipa uzito mkubwa ripoti zinazotokana na Ufuatiliaji na Tathmini katika maamuzi, mijadala na mipango ya Serilikali ili kufikia malengo tarajiwa.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Sakina Mwinyimkuu amesema pamoja na kongamano hilo kuhusisha wataalam na wadau mbalimbali nchini na nje ya nchi, wananchi kwa Ujumla wanaalikwa kupata fursa ya kufahamu namna ambayo serikalini inatekeleza miradi kwani kwa kiasi kikubwa miradi mingi inakwenda kwa wananchi “Mwananchi ndiyo mdau wa kwanza kwani yeye ndo anaweza kujua mradi flani unatekelezwa vizuri katika eneo husika, kwa hivyo tunaona pia ni fursa kwa mwananchi kuweza kufahamu na kutoa hali halisi ya utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.” Alisisitiza.
Kongamano hilo la Pili la Kitaifa la wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika Jijini Arusha linaongozwa na Kauli mbiu inayosema “Kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini kwa ajili ya kujifunza na kuboresha Utendaji wa Serikali.”