Menejimenti ya Wizara ya nishati yakagua maendeleo ya mradi wa JNHPP

Menejimenti ya Wizara ya nishati yakagua maendeleo ya mradi wa JNHPP

General / 1st July, 2022

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakiwa katika picha ya pamoja katika eneo la Tuta Kuu la Bwawa baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere, Juni 28 na 29, 2022 mkoani Pwani.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakipata maelezo kutoka kwa Meneja Usimikaji Mitambo ya kufua Umeme katika Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP), Lewis Simon wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua mradi huo, Juni 28 na 29, 2022 mkoani Pwani.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakipata maelezo wakiwa ndani ya moja ya handaki ambalo ni njia ya kupeleka maji katika mitambo ya kufua umeme, kutoka kwa Meneja Usimikaji Mitambo ya kufua Umeme katika Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP), Lewis Simon wakati wa ziara ya kikazi ya wajumbe hao ya kukagua mradi huo, Juni 28 na 29, 2022 mkoani Pwani.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakitazama hatua ya ujenzi wa nyumba ya kuendeshea Mitambo ya kuzalisha umeme wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Juni 28 na 29, 2022 mkoani Pwani.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakipita katika daraja la kudumu wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Juni 28 na 29, 2022 mkoani Pwani.


Maafisa usafirishaji wa Wizara ya Nishati wakibadilishana mawazo wakati wa ziara ya kikazi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati ya kukagua mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Juni 28 na 29, 2022 mkoani Pwani.

Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wamefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Umeme  wa Julius Nyerere (JNHPP), na kusema kuwa wameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Mradi kulingana na fedha  alizolipwa mkandarasi.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Menejimenti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara, Mkurugenzi wa  Idara ya Sera na Mipango, Petro Lyatuu amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kufuatilia na kukagua utekelezaji wa mradi huo ambao ni mkubwa na wenye maslahi makubwa kwa Taifa.

Lyatuu amesema kuwa, Wizara ya Nishati ni msimamizi mkuu wa utekelezaji wa mradi huo ambapo pamoja na kumuwezesha kifedha mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Wizara inajukumu kubwa la kufuatilia kwa karibu na kutathmini kama malipo ya fedha yanaendana na kazi iliyofanyika.

Amefafanua kuwa, mpaka sasa Serikali imekwishamlipa mkandarasi zaidi ya shilingi Trilioni 4, sawa na asilimia 61 ya fedha anazotakiwa kulipwa mkandarasi huyo kwa kazi iliyokwishafanyika.

“Wizara ni msimamizi Mkuu wa Mradi wa JNHPP na Wakuu wa Idara na Vitengo katika Wizara wana dhamana ya kufuatilia, kukagua, kutathmini na kushauri kuhusu utekelezaji wa mradi huu ili malengo ya mradi yaweze kufikiwa kama ilivyokusudiwa” alisema Lyatuu.

Wajumbe waliofanya ziara hiyo ni Wakuu wa Idara na Vitengo  kutoka Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Idara ya Sera na Mipango, Idara ya Umeme na Nishati Jadidifu, Idara ya Petroli na Gesi, Kitengo cha Ununuzi,  Kitengo cha Sheria,  Kitengo cha Uhasibu, Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, Kitengo cha TEHAMA, Kitengo  cha Mawasiliano Serikalini na Kitengo cha Mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Ziana Mlawa alisema kuwa, Wizara imeweka utaratibu kwa wakuu wa Idara na Vitengo kutembelea miradi inayotekelezwa na Wizara ili kuona na kufahamu  kwa ukaribu kazi wanazozifanya kwa maandishi wawapo ofisini.

Mlawa aliweka wazi kuwa, ziara hizo zinawapa nafasi ya kufahamu changamoto wanazokumbana nazo watumishi wanapotekeleza majukumu yao katika maeneo mengine hasa katika miradi mbalimbali inayotekelezwa mbali na maeneo ya ofisi.

Wajumbe hao wametembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya mradi wa JNHPP ambapo walikagua maendeleo ya ujenzi wa tuta kuu la bwawa, kituo cha kuchochea umeme, nyumba ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme na kingo za bwawa (Saddle Dam)

Pia walikagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la kudumu, Barabara, njia ya kupeleka maji kwenye mitambo ya kuzalisha umeme, nyumba za watumishi pamoja na eneo la ufungaji wa mitambo.

Sambamba na hilo walifanya ziara katika eneo litakalojengwa kituo cha kupoza umeme utakozalishwa katika mradi wa JNHPP na kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini, kilichopo Chalinze mkoani Pwani, pamoja na njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa Kilovolti 400 utakaozalishwa katika mradi huo.