Meli kubwa zaidi iliyobeba Magari 4,041 yatia nanga Dar

Meli kubwa zaidi iliyobeba Magari 4,041 yatia nanga Dar

General / 8th April, 2022

Bandari ya Dar es Salaam imepokea meli aina ya Frontier Ace iliyobeba magari 4,041, ikiwa ni ya kwanza yenye mzigo mkubwa zaidi wa magari kupokelewa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

 

Meli hiyo yenye ukubwa wa GRT 52,276 na urefu wa mita 189.45 imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam leo Ijumaa Aprili 8, 2022 kutoka nchini Japan moja kwa moja, inazidi meli iliyowasili mwaka jana katika bandari hiyo ikiwa na magari 3,743.

 

Agosti 10, 2021 meli nyingine kubwa ya kisasa ilitua nanga bandari ya Dar es Salaam ikiwa na magari 3,743 ambayo yalikuwa ni mengi zaidi kuwahi kusafirishwa kuja nchini kwa mara moja.

 

Meli hiyo ya TRANQUAIL ACE (IMO: 9561253) inayomilikiwa na Kampuni ya Mitsui ikitokea moja kwa moja nchini Japan ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi alisema kuwa meli hiyo imeandika historia mpya kutokana na kubeba shehena kubwa ya magari.

 

Leo, akizungumza wakati wa mapokezi ya meli ya Frontier Ace iliyobeba magari 4,041, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameitaka TPA kuongeza ufanisi katika kupakua mzigo huo pamoja na changamoto ya uhaba wa vifaa uliyopo.

 

Amesema kufanya hivyo kutaongeza imani ya mataifa mbalimbali duniani kutumia bandari ya Dar es Salaam huku akionya kuongezwa uaminifu kwa mizigo ya wateja.

 

"Sio sawa mtu ameletewa gari lake leo anakuta halina kioo, najua tumekuwa tukisifika kwa uaminifu basi hili tuliendeze," amesema Profesa Mbarawa.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi amesema kati ya magari 4,041 yaliyobebwa na meli hiyo 2,936 yatasafirishwa katika nchi za Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, Sudani, Burundi, Msumbiji, Malawi, Uganda, Zambia na Zimbabwe huku mengine 1,105 yakiwa ya wateja wa hapa nchini.

 

Kuhusu ukaguzi wa magari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Balozi Ernest Mangu amesema tayari menejimenti inawasiliana na mamlaka mbalimbali kuhakikisha ukaguzi unafanywa nje ya nchi pekee.