Mdundo na Voko Fursa kwa Vijana
Uzinduzi wa Tamasha la Mdundo na Voko limezinduliwa rasmi hii leo Septemba 3, 2022, huku mgeni rasmi akiwa ni Mkurugenzi wa Idara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Shengoma. Lengo la tamasha hilo ni kuwafikia vijana ambao wanavipaji vya muziki lakini bado hawajapata nafasi ya kutoka kimuziki, lakini pia kuweza kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii zinazowakabili vijana.
Hii sio mara ya kwanza kwa tamasha hili
linaloandaliwa na AFM radio kufanyika nchini, kwani mara ya kwanza lilifanyika
mwaka 2018, ambapo vijana Zaidi ya elfu tatu walifikiwa na walioshiriki ni 205,
kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Dodoma, hata hivyo mwaka 2020/2021 tamasha
halikufanyika kutokana na janga la COVID-19.
Kwa msimu huu Mdundo na Voko, imelenga kuwafikia
vijana kutoka maeneo mbalimbali la jiji la Dodoma, huku kilele chake kikitajwa
kuwa tarehe 26/11/2022, ambapo washindi watajinyakulia zawadi mbalimbali, ikiwa
ni pamoja na kukuza vipaji vyao.
Akieleza juu ya ratiba ya Mdundo na Voko, Ahmed Ally
amesema kuwa tamasha hilo litagusa maeneo ya wilaya ya Bahi, Manyoni, Kondoa,
Gairo, Kibahigwa, Mpwapwa, Kongwa, Dodoma Mjini, na vyuo vyote vya Dodoma, na katika kila
wilaya watachukuliwa washindi watatu, ambao wataingia kambini tarehe 24-25
mwezi wa 11/2022.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Mdundo
na Voko, Mkurugenzi Idara ya Sanaa kutoka Wizara ya Sanaa, Utamaduni na
Michezo, Dkt. Emmanuel Shengoma, amebainisha kuwa wajibu wa serikali katika kuibua
vipaji hivyo ni pamoja na kuanzisha kamati, lengo likiwa ni kuifanya Tanzania
kuwa na mdundo wa aina moja unaotambulisha Taifa.