Mawakala zaidi ya 17,000 NMB kusaidia ukusanyaji kodi ya ardhi nchini.

General / 21st December, 2022

Matawi 228 ya Benki ya NMB nchini katika kila eneo kupitia Mawakala wake zaidi 17,000 watasaidia kutoa huduma za ukadiriaji na ukusanyaji kodi na tozo mbalimbali za ardhi nchini .

Hayo yamebainishwa tarehe 20 Desemba 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula wakati wa uzinduzi wa mkakati maalum wa ushirikiano wa Wizara ya Ardhi na Benki ya NMB katika ukusanyaji wa kodi na tozo mbalimbali za sekta ya ardhi uliofanyika jijini Dar es salaam.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB – Filbert Mponzi alisema wamerahisisha zoezi la kufanya malipo ya sekta ya Ardhi kupitia masuluhisho yao; NMB Mkononi, Mawakala wao waliotapakaa nchi nzima, Mtandao (NMB Direct) na matawi yao yote ili kila mtanzania aweze kufanya malipo kwa wepesi, haraka na salama zaidi.

Dkt Mabula alisema, mkakati wa kushirikiana na Benki ya NMB unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuandaa kampeni maalum ya ukusanyaji kodi na tozo mbalimbali za sekta ya ardhi ambapo wizara yake kupitia NMB na mawakala wao watatoa huduma ya ukadiriaji na ulipaji kodi ya ardhi kwenye matawi 228 ya Benki ya NMB katika kila eneo ambako mawakala zaidi ya 17,000 watatoa huduma hio.

Amesema, Wizara ya Ardhi tayari imetoa mafunzo ya namna ya ukadiriaji na ulipaji wa kodi ya pango la ardhi kwa wafanyakazi wa benki ya NMB kupitia njia ya mtandao ambapo matawi yote yalishiriki. Aidha, mafunzo kwa mawakala yamefanyika katika kila mkoa na zoezi linaendelea.

Amewataka wananchi wote kuchangamkia fursa hiyo ya usogezaji huduma karibu na wananchi na ubunifu uliofanywa kwa kushirikiana na benki ya NMB.

Aidha, Waziri wa Ardhi katika uzinduzi wa kampeni hiyo aligusia pia suala la msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhusiana na riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi ambapo wananchi walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili kusamehewa riba ya malimbikizo na nafuu hiyo ilitolewa kuanzia julai  hadi desemba 2022.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, tangu msamaha huo utolewe takriban miezi mitano na nusu imepita na kasi ya wananchi kujitokeza bado hairidhisha hivyo ametoa rai kwa wananchi wote kutumia kipindi hiki cha siku chache zilizobaki hadi desemba 31, 2022 kusheherekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa furaha ya msamaha wa riba baada ya kukamilisha kulipa deni la msingi ambapo amebainisha kuwa, baada ya muda huo ameelekeza ofisi zote za ardhi kuchukua hatua za kisheria kwa wote wanaodaiwa.

Tembelea tawi lolote ya NMB lilipo karibu nawe au kupitia NMB Mkononi kukamilisha malipo yako kwa wepesi na haraka zaidi.