Matumizi holela ya Dawa hatari kwa Binadamu

Matumizi holela ya Dawa hatari kwa Binadamu

General / 11th April, 2022

Kawaida unaposikia dawa, fikra ya kwanza inayokuja akilini ni uponyaji dhidi ya maradhi. Hata hivyo, dawa hizo badala ya kuwa tiba zinaweza kuwa tatizo endapo zitatumiwa kinyume na utaratibu unavyotaka.

 

Ikiwa ni siku kadhaa zimepita dunia imeadhimisha Siku ya Afya Duniani, Shirika la Afya Duniani (WHO) linabainisha baadhi ya dawa ambazo zinapoteza ufanisi wake kwa kasi kutokana na matumizi holela.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO na wataalamu wengine wa afya nchini, ulaji wa vyakula vya kukaanga ama vilivyo na mafuta mengi kunaweza kusababisha kuumwa na tumbo au kuvimbiwa.

 

Inapotokea hali hiyo, watu hukimbilia duka la dawa na kupata vidonge vya kujitibu bila ushauri wa daktari na hali kama hii hufanywa na watu wengi hususani katika nchi zinazoendelea.

 

Ijapokuwa nchi hizo zina utaratibu wa kudhibiti ununuzi bila ushauri wa daktari, maduka mengi ya kuuza dawa za binadamu hayafuati utaratibu huo wanachojali ni biashara zaidi ya afya ya mteja.

 

Kwa mujibu wa WHO, dawa hizo zinapoteza ufanisi wake kwa kasi kutokana na matumizi mabaya na yasiyo ya kukusudia ya antibiotiki.

 

Lakini dawa hizi zinaweza kuwa na madhara gani kwa afya zikitumiwa bila ushauri wa daktari? Paracetamol ni dawa ambayo hutumiwa na watu wengi kwa ajili ya kutibu maumivu ama homa. Madaktari mara nyingi huagiza paracetamol kwa homa au maumivu ya mwili. Kampuni tofauti huuza kwa majina tofauti.

 

"Tunabainisha jinsi na kwa muda gani wa kula. Lakini baadaye wagonjwa hununua na kula tu wakati wana homa au maumivu ya mwili.

 

Matokeo yake, inapoteza ufanisi wake wakati fulani,” anasema Daktari wa Kituo cha Afya cha Kanisa Katoliki Changombe, Dar es Salaam, Victor Mkalimoto Mkalimoto anasema matumizi ya muda mrefu ya paracetamol au acetaminophen yanaweza kusababisha uharibifu wa ini hivyo elimu zaidi inahitajika ili watu waelewe madhara ya utumiaji dawa bila maelekezo ya daktari.

 

Anasema kuwa matumizi yasiyodhibitiwa ya dawa za kuzuia maumivu au kushindwa kumaliza dozi kunaweza kusababisha hatari kubwa kwa afya ya mwanadamu.

“Aspirin ni dawa muhimu lakini inaweza kuwa hatari ikitumiwa kiholela kwa sababu si salama kwa kila mtu,” anasema Mkalimoto.

 

Naye Daktari wa Kituo cha Afya Lushoto, Michael Mtoi, akizungumza na HabariLEO kwa simu anasema aspirin inajulikana kwa ubora wake wa hali ya juu kutuliza maumivu na wakati mwingine hutumiwa kutuliza homa. Mtoi anasema wazee ambao wana magonjwa ya moyo hupewa dawa hii na madaktari kwa kipimo fulani.

Ikiwa kuna madhara pia hufuatiliwa hivyo ni muhimu kumuona daktari kabla ya kuitumia. Anasema madhara yatokanayo na dawa hiyo yanaweza kusababisha chakula kisisagike vizuri hali ambayo inaweza kumsababishia mtu kupatwa na vidonda vya tumbo. “Usimpatie mtoto aliye na umri wa chini ya miaka 16 aspirin bila ushauri wa daktari.

 

Inaweza kuwafanya watoto kupatikana na ugonjwa hatari unaojulikana kama Reye syndrome ambayo inaweza kuathiri ini au ubongo,” anaeleza Mtoi. Anasema matumizi ya dawa za kupunguza maumivu na uvimbe huchangia ongezeko la hatari ya kupata maradhi ya moyo, utafiti umebaini.

 

Diclofenac na dawa zingine zote zinashauriwa na madaktari hazipaswi kunywewa kiholela kama ambavyo imekuwa ikifanyika katika jamii hivi sasa. Watu wengi hutumia dawa za kutuliza maumivu hasa ya kichwa kama ibuprofen au diclofenac kutoka kwenye maduka ya dawa na kuanza kuitumia bila maelekezo ya daktari.

 

“Inaweza kusababisha matatizo ya tumbo, kuharibu tumbo na kusababisha kutokwa na damu. Mikono na miguu ya watu wengi hutoka maji, huvimba,” anasema Dk John Maula, daktari katika Kituo cha Afya Kisarawe.

 

Anasema matumizi ya muda mrefu ya dawa yanaweza kusababisha kutokwa na damu ya utumbo. Baadhi ya watu wanakabiliwa na mmeng’enyo mbaya wa chakula, wana vidonda na wanaweza kuwa waraibu wa dawa za kulevya.

 

Maula anasema dawa kama vile Ibuprofen, Naproxen na Diclofenac ndizo hutumiwa zaidi kupunguza maumivu na kuondoa kuvimbiwa. Dawa nyingine ambayo inatumiwa vibaya inafahamika kama metronidazole.

 

Anasema baadhi ya watu huzinunua bila maelekezo ya daktari wakiwa na maumivu makali ya tumbo kwani pia ni aina ya dawa ya kutuliza maumivu. Madhara ni pamoja na upele na kuvimbiwa.

 

Kisha yanafuatiwa na shida nyingine kama kutokwa na damu katika sehemu za siri, mgonjwa anapata choo kigumu, ambacho kinasababisha maumivu wakati wa kwenda haja kubwa.

WHO inasema kutokana na matumizi mabaya ya dawa yanaweza kuua watu milioni 300 ifikapo 2050.

 

Baadhi ya watu hununua dawa za tezi au steroid kutoka katika maduka ya dawa kwa matatizo ya koo. Lakini matumizi ya dawa hizo kiholela yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya. Madaktari wametoa ushauri juu ya matumizi ya dawa hizi.

Ikiwa una tatizo la dharura kama vile maumivu, hata ukinunua dawa moja au mbili za dharura dukani, unahitaji kushauriana na daktari haraka iwezekanavyo. Hakuna antibiotics inayopaswa kumezwa kwa ushauri wa wafanyakazi wa maduka ya dawa.

 

Ukiwa na homa, maumivu ya tumbo au tatizo lolote la kimwili, madaktari hawa kwa nyakati tofauti wanashauri upate ushauri wa daktari kabla ya kumeza dawa yoyote kiholela. Angalia madhara na muda wa dawa yoyote kabla ya kutumia na hakikisha unazingatia maagizo ya daktari