Makubaliano ya MIF, Equity Bank na Equit Foundation Kusaidia Elimu ya Kifedha kwa sekta mbalimbali
Na Rajabu Msangi
Taasisi ya Mwanamke Initiative
Foundation, Equity Bank Tanzania pamoja na Equity Group Foundation wameingia
makubaliano yanayolenga kuleta maendeleo kwa mtoto wa kike na vijana kwa
ujumla.
Hayo yamesemwa leo Novemba 21, 2022 na Mwenyekiti wa
Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) ambaye pia ni Mbunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Wanu Hafidh Ameir wakati wa hafla ya
utiaji saini wa Makubaliano hayo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini
Dar es Salaam.
“Mkataba huu utaenda kuiwezesha
Taasisi yetu kuleta maendeleo kwa vijana kwa kuongezea ujuzi kupitia VETA,
itasaidia katika suala zima la nishati na mazingira kuhakikisha kaya zinapata
nishati safi kwa kupikia ili kupunguza uchafuzi wa mazingira” Amesema Mhe.
Wanu.
Aidha amesema Makubaliano hayo
yatasaidia kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo wakike hasa ya kifedha na jinsi
ya kuendesha biashara zao katika kukua na kutengezeza faida.
“Pamoja na hayo, tunaingia
makubaliano ya dhamana ya kupunguza hatari yaani ‘risk’ ya mikopo kwa wajasiriamali
wadogo na wa kati wengi wamekuwa wakishindwa kulipa mikopo yao, sio kwa sababu
biashara ni mbaya bali ni kukosa elimu ya kifedha.
“Katika sekta ya Kilimo,
tutahakikisha wakulima wanakuwa katika mfumo rasmi wa kilimo ili waweze
kuhudumiwa mahitaji yao na kuongezea mnyororo wa thamani wa bidhaa zao”
Ameongeza Mhe. Wanu.
Kwa Upande wake Afisa Mtendaji Mkuu
wa Equity Group, Dkt. James Mwangi amesema Equit Foundation imekuwa ikitumia
njia mbalimbali za kuinua maisha ya watu ikiwemo kuwasaidia watoto yatima
kulipa fedha za shule na mahitaji yao muhimu.
“Huo mpangilio sasa tuna watoto
60,000 ambao tumewapatiaufadhili wa masomo ya sekondari halafu tuna watoto
25,000 ambao tumefadhili elimu ya juu yaani ‘University Education’ na 1000
tumewatuma kutafuta ujuzi na elimu katika mataifa mbalimbali” Amesema Dkt.
Mwangi.
“Mwaka huu peke yake Equity
itatumia Dola za Kimarekani Milioni 60 kulipa gharama za hii mipangilio, kwa
hiyo kwa mwaka ujayo tukisema Mwanamke Initiatives atapata nusu ya hizo fedha,
watu wengi Tanzania watakuwa wamesaidika, tutafikia wengi, tutaelimisha,
tutakuwa na watoto yatima wengi ambao tutakuwa tukilipia ada” Ameongeza Dkt. Mwangi.
Makubaliano hayo yanalenga
kuisaidia Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation katika Elimu ya Kifedha na
mafunzo ya Ufundi Stadi kwa makundi yanayolengwa kutoka sekta mbalimbali kama
vile Kilimo, Afya na Elimu.