Mahakama ya Tanzania yang’ara kimataifa
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linalosimamia masuala ya Miliki Bunifu Duniani (WIPO), Bw. Daren Tang ameitaja
Tanzania kama nchi inayofanya vizuri katika masuala ya ushirikiano na Shirika
hilo ikiwemo kushiriki Mafunzo maalum kwa njia ya masafa marefu yanayoandaliwa
mahsusi kwa Majaji (WIPO Academy Distance Learning General Course on
Intellectual Property for Judges).
Bw. Tang aliyasema hayo hivi karibuni wakati
akifungua Kongamano la Kimaitaifa la Majaji linalojulikana kama ‘WIPO Intellectual
Property Judges Forum’ lililofanyika Makao makuu ya Shirika hilo yaliyopo
Geneva nchini Uswisi huku akikiri kuridhishwa na ushirikiano unaotolewa na
Mahakama ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongozi wa
Mahakama ya WIPO, Bi. Eun Joo Min Tanzania ni nchi ya pili kufanya vizuri
katika ushiriki wa Mafunzo ya masafa marefu ambapo alieleza kuwa Misri
inaongoza kwa kuwa na jumla ya Majaji 300 ikifuatiwa na Tanzania ambapo jumla
ya Majaji na Mahakimu 70 wapo mbioni kuhitimu mafunzo hayo yaliyoandaliwa na
Taasisi hiyo.
Aidha; Bi. Eun aliitaja pia Tanzania kama nchi
mojawapo inayoshiriki kuchapisha maamuzi yanayohusu miliki Bunifu yanayotolewa
na Mahakama ya Tanzania kwenye mtandao wa ‘WIPO Lex Judgment Database’.
Mtandao huo ni maarufu Duniani unamilikiwa na
Shirika hilo huwezesha uamuzi wa Mahakama mbalimbali kusomwa kote duniani. Nchi
zingine zilizoruhusiwa kuchapisha maamuzi yanayotolewa na Mahakama za juu
katika mtandao huo ni Marekani, Uingereza, Hispania, Japan, China, Jamaika, Australia,
Brazil, Korea, Senegal, Togo, Misri, Chile, Gabon, Albania, Congo, Cameroon,
Benin, Burkinafaso, Costa Rica na Ivory Coast.
Kongamano hilo liliwakutanisha zaidi ya Majaji 300
kutoka Nchi mbalimbali Duniani kwa dhumuni la kubadilishana uzoefu wa namna
bora ya utoaji haki kwa siku mbili kuanzia tarehe 16 Novemba, 2022 hadi tarehe
17 Novemba, 2022. Mada Kuu katika kongamano hilo ilikuwa ni Akili Bandia
(Artificial Intelligence) na nafasi yake katika utoaji wa uamuzi.
Mada zingine zilizowasilishwa ni pamoja na Uandishi
wa Hukumu, Hataza na Teknolojia mpya (Patent and New Technology), Utoaji wa
Zuio katika mazingira ya kidigitali, Haki miliki na Teknolijia mpya, nafasi ya
Mahakama katika kuendeleza miliki bunifu na usimamizi wa mashauri.
Miongoni mwa watoa mada katika Kongamano hilo
alikuwa, Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ambaye
aliwasilisha mada kuhusu usimamizi wa mashauri na alitoa uzoefu wa Tanzania
kwenye masuala ya usimamizi wa mashauri yanayohusu miliki bunifu.
Mahakama ya Tanzania ilishiriki katika Kongamano
hilo kwa kuwakilishwa na jumla ya washiriki 22 wakiwemo Majaji 17 na Mahakimu
watano ambapo kati ya idadi hiyo washiriki watatu waliohudhuria ana kwa ana
(physically) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T) ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, Jaji wa Mahakama
Kuu-Divisheni ya Biashara, Mhe. Dkt. Ubena John na Hakimu Mkazi Mwandamizi
ambaye pia ni Mwakilishi wa Mahakama ya Tanzania-WIPO, Mhe. Upendo Ngitiri na
washiriki wengine waliohudhuria Kongamano hilo kwa njia ya mtandao (virtually).
Washiriki hao ni pamoja na Jaji wa Mahakama ya
Rufani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Jaji Mkuu inayosimamia utekelezaji
wa Hati ya Makubaliano kati ya Mahakama ya Tanzania na WIPO, Mhe. Barke Sehel,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim, Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza, Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu-Kanda ya Songea, Mhe. Jose Mlyambina, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni
ya Ardhi, Mhe. Agness Mgeyekwa.
Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya
Sumbawanga, Mhe.Thadeo Mwenempazi, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma, Mhe.
Stephen Magoiga, Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Katarina Revocati
Mteule, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba, Jaji wa
Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Mahimbali, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda
ya Mwanza, Mhe. Lilian Itemba, Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe.
Awamu Mbagwa, Mhe. Jaji wa mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Theodara
Mweneghoha, Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Mtwara, Mhe. Dkt. Eliamini Laltaika
na Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Manyara, Mhe. Gladys Barthy,
Washiriki wengine ni Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu-Kanda ya Temeke, Mhe. Martha Mpaze, Hakimu Mkazi Mwandamizi ambaye pia ni
Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Jovine Constantine, Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Longido, Mhe. Mwajabu Mvungi na Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Bupandwa-Mwanza, Mhe.Amri Katimba.
Ushiriki wa Majaji wa Tanzania katika kongamano ni
sehemu ya utekelezaji wa Hati ya Makubaliano iliyosainiwa tarehe 05 Machi, 2021
kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WIPO, Bw. Daren Tang na Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma.
Shirika la WIPO lilianza kushirikiana kwa karibu na
Mahakama ya Tanzania tangu mwaka 2018 ambapo hivi sasa wanashirikiana katika
mambo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa majumuisho ya sheria na maamuzi yanayohusu
miliki bunifu, uaandaji wa nyenzo za kufundishia (Training Materials) na
Utatuzi wa Migogoro kwa njia usuluhishi.
Shirika hilo linashirikiana pia na Mahakama katika kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu katika eneo la miliki bunifu kupitia mafunzo maalum na ushiriki wa Maafisa hao wa Mahakama katika mikutano, semina na makongamano mbalimbali yanayoandaliwa na Shirika hilo.
Washiriki kutoka nchi mbalimbali walioshiriki Kongamano la Kimaitaifa la Majaji linalojulikana kama ‘WIPO Intellectual Property Judges Forum’. Tanzania ni moja kati ya Nchi zilizoshiriki katika Kongamano hilo lililofanyika hivi karibuni Geneva-Uswisi.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Miliki Bunifu Duniani (WIPO), Bw. Daren Tang akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimaitaifa la Majaji linalojulikana kama ‘WIPO Intellectual Property Judges Forum’ lililofanyika hivi karibuni Geneva nchini Uswisi.
Washiriki Wanawake wakiwa katika picha ya pamoja katika Kongamano la Kimaitaifa la Majaji nchini Geneva.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha IJA -Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akitoa uzoefu wa namna mashauri yanavyosimamiwa katika Mahakama za Tanzania.
Sehemu ya Washiriki wa Kongamano hilo kutoka Mahakama ya Tanzania, kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Dkt. Ubena John na katikati ni Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mwakilishi wa Mahakama ya Tanzania katika Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO), Mhe. Upendo Ngitiri.
Sehemu ya Washiriki kutoka Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongozi wa Mahakama ya WIPO, Bi. Eun Joo Min (kushoto), Mwanasheria wa WIPO, Bi. Ines Ferdinandez (wa pili kushoto) na Mwanasheria wa WIPO, Bi. Nahal Zerbajadi (kulia).
(Kutoka Maktaba) Katika picha ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa WIPO, Bw. Daren Tang wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Shirika hilo, hafla ya utiaji saini ilifanyika tarehe 05 Machi, 2021.