Maendeleo Bank yapata faida Bilioni 1.3 mwaka 2022

General / 31st January, 2023

Benki ya Maendeleo imepata faida kutoka Shilingi milioni 580 hadi Shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka 2022 kutokana  na kuwepo kwa njia sahihi za uzalishaji.

Hayo yamesemwa na leo Januari 30, 2023 na Mkurugenzi wa Maendeleo Bank, Ibrahimu Mwangalaba wakati akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Benki hiyo  kwa mwaka uliopita mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam .

Aidha amesema  Benki hiyo imekuwa ikiwaandaa wajasiriamali wanawake, vijana na wamachinga katika namna bora ya kupatiwa elimu ya mikopo itakayowawezesha kuboresha mitaji yao na jinsi ya kulipa kwa urahisi ili kuepuka changamoto za ulipaji.

“Pamoja na hayo benki inakusudia kutoa bidhaa kwa ajili ya wamama na vijana, na kuwafundisha namna ya kuendesha mikopo hiyo na watapata kutokana vigezo ambavyo tutavizingatia,” amesema Mwangalaba.

Mwangalaba amesema kuwa mpango wa kuwapa mikopo wamachinga ulianza mwaka uliopita. ambapo kiasi cha Sh bilioni 3 zilitumika kwa wamachinga 2500, hivyo kutokana na mafanikio mwakubwa ya mwaka 2022 wameamua kuongeza makundi ya wanufaika.

Wakati akibainisha lengo la benki hiyo amesema lengo la benki hiyo ni kuwafikia wamachinga 5000 na kufafanua kuwa zaidi ya wanawake 3000 tayari wamefikiwa, na wamepanga kuwapa elimu wanawake zaidi ya 15,000 ambao watanufaika na mikopo.

Kwa upande wa mikakati ya benki hiyo mwaka 2023 Mwangalaba ameongeza kuwa  wamepanga kuongeza matawi kwenye baadhi ya maeneo kabla ya Aprili mwaka huu, pamoja na kuanzisha huduma za mitandao ‘Sim Banking’ na namna nzuri ya ulipaji ada kwa wanafunzi.