KUKOSA MISIMAMO KUNAWAGHARIMU CHADEMA

KUKOSA MISIMAMO KUNAWAGHARIMU CHADEMA

General / 16th October, 2024

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Chadema imekuwa ikitoa matamko yenye kuashiria misimamo mikali kuhusu ushiriki wao kwenye uchaguzi bila katiba mpya. Mei 2021, mwenyekiti Freeman Mbowe alitangaza kwa ukali: “Bila katiba mpya, hatushiriki uchaguzi wowote.” Msimamo huu ulirudiwa tena Februari 2023 na makamu mwenyekiti Tundu Lissu aliposema, “Bila katiba mpya, Chadema haitashiriki uchaguzi mkuu 2025.”


Hata hivyo, hali imegeuka. Kufikia Disemba 2023, katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika, alitangaza kuwa maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025 yalikuwa yakiendelea. Msimamo ukabadilika rasmi Julai 2024, pale ambapo Mbowe alitangaza kuwa “Hatuta susia uchaguzi. Tuta pambana kuwatoa madarakani.” Kisha, Oktoba 2024, Godbless Lema akaibua tuhuma kuwa CCM ilikuwa ikiandikisha wanafunzi kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa.


Chadema, chama ambacho kwa miaka mitatu kilionekana kuweka matumaini yote katika mchakato wa katiba mpya, sasa kimebadili msimamo bila maandalizi ya kutosha. Wakati waliposema hawatashiriki chaguzi bila katiba mpya, walijenga matumaini makubwa kwa wafuasi wao, lakini leo hii wamesalimu amri bila kutimiza sharti hilo waliloliweka.


Kutokana na mabadiliko haya ya ghafla, Chadema sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa—ikiwa maandalizi yao kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa yanaonekana kuwa na mapungufu, uchaguzi mkuu wa 2025 unaweza kuwa janga kwao. Wameanza kutoa visingizio hata kabla ya uchaguzi, hali inayoashiria ukosefu wa maandalizi thabiti na utayari wa kukabiliana na CCM kwenye uchaguzi. Hii ni dalili ya chama kinachokosa mwelekeo na msimamo madhubuti, jambo ambalo linaweza kuwa na athari kubwa kwao.