Kilele Maadimisho Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi Kufanyika Morogoro
Tanzania inatarajia kuungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya usalama na afya mahala pa kazi
Hayo yamebainishwa leo
April 26, 2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, Vijana, Ajira na
wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako wakati akizungumza na waandishi wa habari
Jijini Dodoma.
Amesema maadhimisho
hayo yameanza rasmi leo yakiambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo uhamasishaji,
Maonesho na mafunzo ya usalama na afya kwa wafanyakazi, utoaji tuzo pia yatawakutanisha wamiliki na wasimamizi
sehemu za kazi, lengo likiwa ni kutafakari kuhusu usalama wa kazi na
kuwakumbuka walioumia au waliopoteza maisha wakiwa katika utekelezaji wa
majukumu yao
Aidha, ametanabaisha kuwa takwimu za kidunia zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani mwaka 2022 zinaonesha kwamba zaidi ya watu milioni mbili na laki tisa (2.9) hupoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, Kwa upande wa Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249 katika ajali hizo, vifo vilikuwa 217.
Aidha, Prof. Ndalichako amewataka waajiri, wafanyakazi na wananchi wote kwa ujumla kushiriki katika maadhimisho hayo ambayo kitaifa yatafanyika April 28, 2023 mkoani Morogoro, yakiongozwa na Kaulimbiu “Mazingira Salama na Afya Kazini ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahala pa kazi”, kaulimbiu inayotokana na Azimio la Wanachama wa Shirika la kazi Duniani (ILO) katika kikao cha Juni 2022 kilichofanyika huko Geneva Uswisi, na kuamua kuwa suala Usalama na Afya mahali pa kazi liwe mojawapo ya Kanuni na Haki tano za msingi kwa wafanyakazi mahali pa kazi,"
Nae Mtendaji Mkuu wa
OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema kuwa ajali nyingi zinaripotiwa ni katika sekta ya
Uzalishaji ambapo imeajiri vijana wengi huku wengine wakiwa hawana ujuzi wa
kutosha katika nafasi wanazofanyia kazi.
"Uzalishaji lina
matukio mengi ya ajali na hii ni kutokana na vijana wengi kujikita katika eneo
hilo kujiajiri ama kuajiriwa huku wengine wakifanya tu bila kuwa na ujuzi wa
kutosha au taaluma kwani eneo hilo mara nyingi wanaangalia nguvu sana kuliko
taaluma ndio maana ajali zinakuwa nyingi," amesema Bi.Mwenda
Siku ya Usalama na Afya
Mahali pa Kazi Duniani ilianza mwaka1996 Nchini Marekekani Katika Jiji la New
York, ambapo waathirika wa watu walioumia na kupoteza maisha
wakiwa kazini hukumbukwa. Maadhimisho hayo yalikuwa yakifanywa na
Chama Cha Wafanyakazi Duniani. Ilipofika mwaka 2001,Shirika la Kazi Duniani
liliona kuwa ni busara kubadilisha madhumuni ya siku hiyo na kuiita “Siku
ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani”.