Kamati ya kudumu ya bunge PIC yatembelea Miradi mitatu ya NHC Dar

General / 30th April, 2023

Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imefanya ziara katika miradi mitatu inayosimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa NHC ambayo ni Mradi wa Moroco Squares, mradi wa Seven Eleven na Mradi wa Samia Housing iliyopo Mkoani Dar es Salaam.  


Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jerry Silaa amesema hatua hiyo imekuja baada ya Shirika la Nyumba kujadili na kamati na kuona baadhi ya miradi iliyokwama lakini kwa sasa miradi hiyo inaendelea chini ya usimamizi wa shirika la Nyumba la Taifa.


"Kwanza nimpongeze Rais Samia kuweza kuifufua miradi hii, mahitaji ya nyumba Tanzania bado yapo juu sana, wataalam hawa watakwambia". Amesema Silaa.


Aidha Silaa amesema kwa niaba ya kamati watahakikisha serikali inaunga mkono kwa mashirika wanapokuwa wanatekeleza miradi yao.


"Mashirika haya ya umma yameundwa kutengeneza faida, kwa hiyo tunavyounda shirika tunaunda wakurugenzi, tunaweka bodi, aakati mwingine tuiamini na tuache ifanye mipango yao iliyojiwekewa na sheria ya bunge ili wafikie malengo bila kuwa na mwingiliano." Amesema Silaa.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC Hamad Abdallah amesema shirika litahakikisha miradi yote inayojengwa itazingatia kuendana na teknolojia inavyokuwa huku akiongeza miradi hiyo itaendelea kuzalisha ajira kwa watanzania.


"Mradi huu wa Samia Housing tayari tumeshuuza kwa asilimia 80, maana yake kuna kiu kikubwa sana cha makazi kwa Dar es Salaam lakini pia maeneo mengine ya Tanzania. "


"Tumeajiri watanzania, kwa sasa tumeajiri ajira Mia tatu lakini hivi karibuni tutaanza kwenda usiku na mchana maana yake mchana tunaweza kuwa na waru takribani 500 na usiku 500 mwisho wa siku tunaweza kuwa na ajira 1000 ambazo zitakuwa zimezalishwa na mradi huu." Ameongeza Bw. Hamad.