Fedha za Sherehe za Mapinduzi Kuboresha Elimu Zanzibar

General / 9th January, 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt Selemani Jafo, amesema kuwa hakutakuwa na sherehe kubwa za maadhimisho ua Mapinduzi Katika uwanja wa Amani kama ilivyoelekezwa hapo awali na badala yake fedha zilizopangwa kuadhimisha sherehe hizo zitaelekezwa katika miradi mbalimbali ya sekta ya elimu Zanzibar.


"Fedha hizi zinakwenda kutumika kuongeza madarasa, madawati, maabara na huduma nyingine za elimu visiwani Zanzibar vilevile yatahusisha ukaguzi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekezaji katika sekta mbalimbali chini ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar" Amesema Jafo.


Hayo yamebainishwa leo Januari 9, 2023 na Waziri Selemani Jafo, wakati akizingumza na waandishi wa habari Katika mji wa Kiserikali Mtumba, Dodoma kuelekea maadhimisho ya mapinduzi ya Z'bar tarehe 12 January 2023.


Aidha, katika kuadhimisha sherehe hizo, Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira imejipanga kuadhimisha sherehe za mapinduzi ya Zanzibar kwa kupanda miti katika viunga na maeneo mbalimbali Jijini Dodoma.



Ameongeza kuwa Januari 11, 2023 zoezi la upandaji miti litaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt Pindi Chana katika Bwawa la Swaswa wakati Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Sinyamule ataongoza zoezi hilo katika eneo la wazi la Chidachi. 



“Mtakumbuka kuwa Serikali ilielekeza mwaka huu wa 2023 hakutakuwa na sherehe kubwa za maadhimisho ya Mapinduzi, katika Uwanja wa Amani kama ilivyozoeleka, badala yake gharama zilizopangwa kuadhimisha sherehe hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imeazimia kudhimisha sherehe hizo kwa kuendeleza shughuli ya upandaji miti katika viunga na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma,” amefafanua.



Aidha, amewapongeza viongozi wa awamu zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika nyanja mbalimbali katika kuleta maendeleo endelevu kwa jamii ya pande zote za Muungano.



Akitoa pongeza kwa wadau mbalimbali Dkt. Jafo amesema shughuli za upandaji miti ni katika kuendeleza azma ya Serikali kuifanya Dodoma kuwa ya kijani inayopendeza na kuvutia huku akitoa wito wa kuyshiriki kwa pamoja.



Hivyo, amewataka Watanzania wote Bara na Zanzibar kupanda miti katika makazi yao na kuendelea kuitunza hadi ikue na kuongeza uoto wa asili katika nchi yetu.

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huadhimisha na Kuenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Kila ifikapo tarehe 12 Januari kila mwaka, kwani mapinduzi hayo yalitokea mnamo tarehe 12, Januari 1964, ambapo utawala wa Sultan uliondolewa na kutoa uhuru kamili kwa watu wa Zanzibar.