Dkt. Tulia: Andaeni taarifa ya waliohusika kuwapa ujauzito wanafunzi"

Dkt. Tulia: Andaeni taarifa ya waliohusika kuwapa ujauzito wanafunzi"

General / 31st January, 2023


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Akson amemtaka Naibu Waziri kuandaa taarifa juu ya idadi ya watu waliohusika kuwapa ujauzito wanafunzi na tayari wamefikishwa mahakamani na kukutwa na hatia.


Dkt. Tulia ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma baada ya taarifa iliyotolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipangaa wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa viti maalum Hawa Mchafu Chakoma kuhusu idadi ya wanafunzi waliokatisha masomo yao kwa mwaka 2022.


"Taarifa hii ni muhimu sana kwani itasaidia kujua kama sheria yetu inawalinda kweli hawa watoto dhidi ya hivyo vitendo viovu au hapana, na kama tunahitaji kufanyia marekebisho ili hao watu takwimu badala ya kukuwa ziwe zinapungua" amesema Spika Tulia.


Naibu Waziri  Kipanga amesema takribani wanafunzi 1554 wa shule ya msingi na wanafunzi 7457 shule za Sekondari nchini wameripotiwa kukatisha masomo yao katika kipindi cha mwaka 2022 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.


Ameongeza kwa kusema kuwa katika idadi hiyo ya wanafunzi waliokatisha masomo ni wanafunzi 1692 pekee wa shule za sekondari ambao wamerejea shule na kuendelea na masomo, huku kwa shule za msingi bado taarifa zinaendelea kukusanywa ili kufahamu ni wanafunzi wangapi wamerejea shuleni.

Aidha, Naibu Waziri amebainisha juu ya mikakati ambayo serikali imeweka kuhakikisha inazuia suala hilo, kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule 26 za wasichana kila mkoa kwa awamu tofauti ambapo mpaka hivi sasa tayari shule 10 zimeanza kujengwa katika awamu ya kwanza, ujenzi wa mabweni lakini pia kuanzisha vitengo vya elimu na unahisi katika shule pamoja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaohusika kukatisha masomo wanafunzi.