CRDB Yatoa Ubalozi kwa Wachezaji Simba na Yanga Kampeni ya "Benki ni SimBanking "

CRDB Yatoa Ubalozi kwa Wachezaji Simba na Yanga Kampeni ya "Benki ni SimBanking "

General / 23rd February, 2023

Benki ya CRDB imesaini mkataba wa makubaliano na wachezaji Clatous Chama, Mohammed Hussein, Aziz Ki na Farid Mussa kutoka Simba na Yanga kuwa mabalozi wake wa kufikisha elimu ya fedha kwa jamii kupitia kampeni yake ya “Benki ni SimBanking.”

Mikataba na wachezaji hao imesainiwa katika makao makuu ya Benki ya CRDB na kushuhudiwa na viongozi waandamizi kutoka Benki ya CRDB pamoja na vilabu vya Simba na Yanga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela amesema Benki ya CRDB kwa muda mrefu imekuwa ikishiriki katika kusaidia jitihada mbalimbali za kimichezo kwa kutambua mbali ya kuwa michezo ni burudani, bali pia michezo ni biashara na uchumi pia. 

 
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Benki ya CRDB imeanzisha mbio za kimataifa za hisani za CRDB Bank Marathon, mashindano ya taifa ya mpira wa kikapu ya CRDB Bank Taifa Cup pamoja na mashindano ya resi za Ngalawa ya CRDB Bank Ngalawa Race.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine ameishukuru Benki ya CRDB kwa kutoa ubalozi kwa wachezaji wao jambo ambalo litaleta hamasa kwa wachezaji wengine kuongeza juhudi jambo ambalo litaisadia klabu wakati huu inaposhiriki mashindao ya ndani nan je ya nchi. Mtine alisema Klabu ya Yanga inafarijika pia kuwa sehemu ya familia ya Benki ya CRDB kwa kusaidia kufikisha elimu ya fedha katika jamii, na kuwaletea wananchi maendeleo.

“Tunaishukuru Benki ya CRDB kwa kuwatambua wachezaji wetu na kuwapa heshima hii kubwa ya kuwa mabalozi wao. Kwa kuwa mabalozi wa taasisi kubwa kama Benki ya CRDB kunaleta imani na hamasa hata kwa taasisi nyingine kutaka kushirikiana na wachezaji wetu jambo ambalo litanuifaisha sio tu wachezaji bali vilabu na soka letu kwa ujumla wake” alsema Mtine.

Akizungumza kwa upande wa klabu ya Simba, Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula na yeye amepongeza hatua ya Benki ya CRDB kuwatambua wachezaji wao na hasa kwa kuangalia mchango wao katika timu na nidhamu jambo ambalo ni muhimu kwa mafanikio yao na timu kwa ujumla. Aidha, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo, na kuahidi kuendelea kushirikiana kupitia kampeni hiyo ya Benki ni SimBanking.

“Pamoja na kuwa mikataba hii inakwenda kuongeza kipato kwa wachezaji lakini kupata nafasi ya kupewa elimu ya fedha ambayo itawasaidia kwenye maisha yao wakati huu wanacheza soka la ushindani na wakati ambao watakua wamestaafu ni jambo kubwa na la kupongezwa kwani wachezaji wengi wameshindwa kunufaika na vipaji vyao kwa kukosa elimu ya fedha” aliongeza Kajula ambae amewahi kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za fedha nchini.