CRDB yatakiwa kuharakisha Matumizi ya Mfumo wa Malipo wa GePG -Burundi

CRDB yatakiwa kuharakisha Matumizi ya Mfumo wa Malipo wa GePG -Burundi

General / 24th February, 2023

Benki ya CRDB imetakiwa kuharakisha matumizi ya mfumo wa malipo ya Serikali kwa njia ya kieletroniki (GePG) ili kuongeza na kuharakisha shughuli za kiuchumi kati ya Tanzania na Burundi.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba wakati alipotembelea na kufanya kikao na  Menejimenti ya Benki hiyo mjini Bujumbura nchini Burundi, ambako Benki hiyo inatoa huduma za kibenki kwa miaka kumi sasa.

Mhe. Nchemba alisema kwamba amefarijika kusikia mchakato wa kuanza kwa matumizi ya ‘’control number’’ kwa ajili ya malipo ya ushuru kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na uondoshaji mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam upo katika hatua za mwisho.

Alisema kuwa kukamilika kwa matumizi ya mfumo huo wa malipo ya Serikali kwa njia ya kieletroniki kutasaidia kupunguza usumbufu na hasara wanayopata wanafanyabiashara wa Burundi wanapotaka kulipia mizigo yao inayopita katika Bandari za Tanzania.

‘’Nimefarijika sana niliposikia hilo la ‘contorl number’ kuwa litafanyika huku huku Burundi kwa sababu litawezesha na kuharakisha shughuli za kiuchumi na hicho ndicho kitu kikubwa ambacho Viongozi wetu wamekuwa wakikitaka na kukitamani kifanyike haraka’’ alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Aliongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye wamekuwa wakihimiza urahisishaji wa ufanyaji biashara kati ya nchi hizi mbili, hivyo ni vema matumizi ya ‘control number’ yakaanza haraka ili kurahisisha ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax ambaye aliongozana na Mhe. Dkt. Nchemba kwenye ziara hiyo, aliipongeza Benki hiyo kwa hatua waliyoichukua ya kutoa huduma za kibenki nje ya Tanzania jambo ambalo linaitangaza Tanzania na kurahisisha ufanyaji wa biashara kwa Watanzania wanaokuja Burundi na Warundi wanaofanya biashara na Tanzania.



Dkt. Tax ameisihi benki hiyo kupanua huduma zao ili zienee kote nchini Burundi na kuvuka mipaka hadi katika nchi ya Jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na si kuishia katika jiji la Bujumbura pekee.