Chuo cha ufundi Dodoma kuanza kudahili Januari 2023

Chuo cha Ufundi Dodoma kilichopo eneo la Nala kinatarajiwa kuanza udahili Januari 2023 ambapo katika awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 kwa wakati mmoja.
Hayo yamesemwa Jana Februari 28, 2022 Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) wakati akiwa katika ziara mkoani humo ambapo amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa Chuo hicho utagharimu Shilingi bilioni 17.9
Amefafanua kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa chuo hicho itakuwa na majengo 18 na unatarajia kukamilika Desemba mwaka huu.
"Chuo hiki kikikamilika kabisa kitaweza kuchukua wanafunzi 1,500 watakaokaa hosteli na wengine zaidi watakaokaa nje ya chuo," ameongeza Mhe. Kipanga.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Kipanga pia ametembelea Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mfano Iyumbu ambapo ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa Mradi huo ambao ulitakiwa kukamilika Februari 22, 2022 lakini mpaka leo ujenzi wake umefikia asilimia 62.
"Kwa kweli hatujaridhishwa na ucheleweshaji huu, tunaenda kukaa pande zote kujadili nini cha kufanya ili kuwezesha mradi huu kukamilika," amesema Naibu Waziri Kipanga.
Naye Luteni Kanali Filemon Komanya akiongea kwa niaba ya mkandarasi wa mradi huo, Suma JKT amesema kuwa changamoto mbalimbali zimepelekea kuchelewa kukamilika kwa mradi huo ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya ujenzi, hali ya hewa ya mvua na fedha.
Amesema wameiomba Wizara kuwaongezea muda wa miezi sita ili waweze kukamilisha ujenzi huo.