Benki ya NMB yaingia makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati na K-FINCO ya Korea Kusini
Benki ya NMB leo imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) ya kushirikiana na Shirika la Korea Kusini linalojihusisha na kudhamini miradi katika sekta ya ujenzi la Korea Finance for Construction (K-FINCO).
Lengo la makubaliano hayo ni kusaidia kuwawezesha wakandarasi wa Korea Kusini kushiriki kikamilifu katika miradi ya ujenzi nchini Tanzania ambapo NMB itaiwakilisha K-FINCO kwa kutoa dhamana za kupata zabuni za kutekeleza miradi hiyo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Benki ya NMB na K-FINCO zitakuwa na jukumu muhimu la kuvutia miradi mikubwa ya ujenzi itakayosaidia kuboresha maisha ya Watanzania. Ushirikiano huu pia unatarajiwa kuendeleza ukuaji wa mitaji, kutengeneza ajira, na kuifanya Tanzania kuwa kinara wa miundombinu katika ukanda huu.
Hafla ya utiaji saini ya ushirikiano huo imeshuhudiwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mheshimiwa Togolani Mavura. Ujumbe wa NMB uliongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO), Bi Ruth Zaipuna, huku ujumbe wa K-FINCO ukiongozwa na Dkt. Eunjae Lee, ambaye ni CEO wa taasisi hiyo na mwenyekiti wa bodi yake ya wakurugenzi.
Mkataba huo, ambao unatarajiwa kuimarisha maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini, unazichagiza taasisi hizo mbili kufanya kazi kwa karibu zaidi ili kuchangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa Tanzania na jitihada za ujenzi wa Taifa.
Tunaimani kuwa hatua hii itaimarisha mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na Korea Kusini, na kukuza urafiki kati ya wananchi wa mataifa haya mawili.