Wenye Viwanda watakiwa kuongeza Uzalishaji

Wenye Viwanda watakiwa kuongeza Uzalishaji

General / 20th November, 2022

Na Rajabu Msangi

Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango akiwa na viongozi wa Kiwanda cha Tanga Cement ambao waliibuka washindi wa jumla kwenye tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Mwaka PMAYA, zilizofanyika Jumamosi Serena jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).


Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango amevitaka viwanda kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya ndani na kupunguza upotevu wa Rasilimali ya fedha za kigeni.

Dkt. Mpango ametoa wito huo wakati akikabidhi tuzo za mzalishaji bora wa mwaka ambazo zinaandaliwa kila mwaka na Shirika la Wenye Viwanda Nchini (CTI)

" Naomba nitumie fursa hii kuhimiza  wenye viwanda wote hapa nchini mfanye jitihada na kuongeza uwezo wa uzalishaji katika viwanda vyenu ili kukidhi mahitaji ya ndani na hivyo kupunguza upotevu huu wa rasilimali hii ya fedha za kigeni" alisema Dkt. Mpango


“Nilipokutana nanyi mwaka jana nilieleza kutofurahishwa na ongezeko la uagizaji wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa humu nchini. Changamoto hii bado ni kubwa kwa mfano, takribani asilimia 12 ya fedha za mauzo nje ya nchi zinatumika kulipia uagizaji wa bidhaa za walaji  ambazo nyingi tunaweza kuzalisha wenyewe hapa nchini na kwa mwaka unaoishia Septemba 2022, tumetumia takribani dola za Marekani milioni 346 kuagiza mbolea,” ameongeza Dkt. Mpango.

Aidha amesema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji hapa nchini kwa kufanya maboresho zaidi ya kitaasisi, sheria, sera za fedha na bajeti na kwamba hadi sasa, zaidi ya kodi na tozo 230 zisizo na tija zimefutwa na takribani sheria na miongozo 40 imeboreshwa na majukumu ya baadhi ya taasisi yameendelea kuboreshwa ili kuongeza ufanisi.

“Sambamba na hili, tunadhamiria pia kuiunganisha reli yetu na nchi jirani kama Burundi na DRC ili kuchochea biashara ya kikanda na kuwezesha Taifa kunufaika na huduma (logistics) na usafirishaji wa madini na bidhaa mbalimbali kutoka katika nchi hizo,” amesema.

Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango, akimkabidhi tuzo mshindi mwingine hafla ya kuwazawadia washindi wa tuzo ya mzalishaji bora wa mwaka viwandani (PMAYA) inayoandaliwa kila mwaka na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI).


Katika hatua nyingine ameongeza serikali inaendelea na jitihada za upanuzi na kuongeza ufanisi wa Bandari kuu za Dar es salaam, Mtwara na Tanga pia Bandari katika Maziwa Makuu na kuimarisha mfumo wa forodha kwa ajili ya upitishaji na utoaji wa mizigo kwa haraka. 

Dk. Mpango amesema hatua hizi zote zimeleta matokeo chanya na kuendelea kuvutia idadi kubwa ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi akitolea mfano wa  mwaka 2021 miradi iliyosajiriwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) ilikuwa 256 ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 3.7 kutoka 208 mwaka 2020 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.1.